AZAM YAIFUNGA SIMBA NA KUTINGA FAINALI YA KOMBE LA MAPINDUZI


Wachezaji wa Azam wakiwa wamembeba shujaa wao wa leo Malika Ndeule

Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
AZAM FC imeingia Fainali ya Kombe la Mapinduzi usiku huu, baada ya kuifunga Simba SC kwa penalti 5-4, kufuatia sare ya kufungana mabao 2-2 ndani ya dakika 120 usiku huu kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani hapa.
Hadi mapumziko, Azam FC walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na kiungo Mkenya, Humphrey Mieno dakika ya 10, akiunganisha kwa kichwa kona maridadi iliyochongwa na kiungo mzalendo, Ibrahim Mwaipopo.
Azam ilishambulia zaidi baada ya bao hilo, kabla ya Simba kuzinduka dakika tatu baadaye na kuanza kushambulia pia.
Mchezo huo ulisimama kwa dakika tano kuanzia ya 14 hadi 19 kutokana na umeme kukatika uwanjani hapo, hali iliyolazimisha kuwashwa kwa Jenereta.
Kipindi cha pili Simba walibadilika mno kiuchezaji na kuanza kutawala mchezo jambo ambalo liliwasaidia kupata bao la kusawazisha dakika ya 78, ambalo lilifungwa na Rashid Ismail.
Simba ilipoteza nafasi mbili za wazi za kufunga mabao ndani ya dakika 45 za kipindi cha pili na mchezo ukamalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1.
Katika dakika 30 za nyongeza, Simba walifanikiwa kupata bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 110, mfungaji Miraj Madenge.
Azam walionekana kupagawa baada ya kupigwa bao la pili na kuanza kucheza rafu za ovyo na kutoa maneno machafu kwa refa, jambo ambalo liliwaponza kupoteza wachezaji wawili ndani ya dakika mbili.
Refa Waziri Shekha alianza kumtoa nje kwa kadi nyekundu kiungo Mwaipopo dakika ya 114 na baadaye Jabir Aziz dakika ya 116.  
Wakati refa huyo akijiandaa kupuliza kipyenga cha kuhitimisha mchezo na mashabiki wa Simba wakiwa wameuteka Uwanja wa Amaan kwa shangwe zao, beki Emily Mgeta alimuangusha kwenye eneo la hatari beki Malika Ndeule na hivyo kuwa adhabu ya penalti.
Malika amebebwa juu juu
Beki Mkenya, Joackins Atudo ambaye amekuwa akipewa dhamana ya kupiga penalti kwa sasa Azam FC, alikwenda kupiga mkwaju huo na kuukwamisha nyavuni kuwapatia Watoto wa Bakhresa bao la kusawazisha.
Kutoka hapo, mchezo ulihamia kwenye mikwaju ya penalti na usiku huu bahati haikuwa yake kiungo matata chipukizi wa Simba, Haroun Athumani Chanongo, kwani pamoja na kupiga penalti nzuri iliyokuwa ya pili kwa timu yake, iligonga mwamba wa juu katikati na kudunda chini kisha kurejea uwanjani.
Wachezaji wa Simba waliofunga penalti zao leo ni Komabil Keita ya kwanza, Jonas Mkude ya tatu, Miraj Adam ya nne na Ramadhani Mkiparamoto ya tano, wakati wa Azam waliofunga ni Gaudence Mwaikimba ya kwanza, Himid Mao ya pili, Atudo ya tatu, Samir Hajji Nuhu ya nne na Malika Ndeule ya tano.
Kwa matokeo hayo sasa, Azam itamenyana na mshindi wa kesho kati ya Tusker na Miembeni katika fainali Jumamosi.
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; William Mweta, Miraj Adam, Paul Ngalema, Hassan Khatibu/Hassan Isihaka dk89, Komabil Keita, Jonas Mkude, Ramadhani Singano/Miraj Madenge dk71, Abdallah Seseme/Said Demla dk 61, Rashid Ismail, Marcel Kaheza/Ramadhan Mkipalamoto dk72 na Haroun Chanongo.
Azam FC; Mwadini Ally, Himid Mao, Samir Hajji Nuhu, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Seif Abdallah/Gaudence Mwaikimba dk69, Ibrahim Mwaipopo, Brian Umony/Malika Ndeule dk104, Humphrey Mieno/Jabir Aziz dk79 na Uhuru Suleiman. 


Mgeni rasmi, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho akisalimiana na kipa wa Azam FC, Mwadini Ally katika mchezo wa leo wa Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba SC kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Azam ilishinda kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 120.

Kikosi cha Simba leo

Kikosi cha Azam leo

Kipre Balou wa Azam kulia akiwania mpira wa juu na Abdallah Seseme wa Simba

Samir Hajji Nuhu wa Azam akiwatoka wachezaji wa Simba

Miraj Adam wa Simba akiuwahi mpira dhidi ya Hajji Nuhu wa Azam

Humphrey Mieno wa Azam aliyeenda hewani kuifungia bao la kwanza timu yake 

Wachezaji wa Azam, Ibrahim Mwaipopo kushoto na Uhuru Suleiman kulia wakimdhibiti kiungo wa Simba SC, Ramadhani Singano 'Messi' katikati huku kocha wake Jamhuri Kihwelo 'Julio' kulia kabisa akishuhudia

Wachezaji wa Azam wakimpongeza Humphrey Mieno kufunga bao la kwanza

Paul Ngalema wa Simba akimdhibiti Uhuru Suleiman wa Azam FC

Ibrahim Mwaipopo anatoa pasi huku akiwa amebanwa na wachezaji wa Simba SC

Kipa wa Simba SC, William Mweta akiwa amedaka mbele ya mshambuliaji wa Azam, Brian Umony huku beki wake Paul Ngalema akiwa tayari kutoa msaada kulia

Seif Abdallah wa Azam akiwatoka mabeki wa Simba

Ramadhani Mkipalamoto akiwatoka mabeki wa Azam

Kipre Balou akimiliki mpira mbele ya Jonas Mkude wa Simba

Haruna Chanongo akitoa pasi kwa kichwa mbele ya Ibrahim Mwaipopo

Miraj Madenge wa Simba, akimiliki mpira mbele ya Himid Mao wa Azam

Himid ameosha mbele ya Madenge

Madenge akimpongeza Rashid Ismail kufunga bao la kwanza la Simba SC

Mwadini Ally amedaka mbele ya beki wake Himi Mao, huku Ramadhani Mkipalamoto akifukuzia

David Mwantika wa Azam akimdhibiti Mkipalamoto wa Simba SC

Samih Hajji Nuhu amempitia Mkipalamoto na mpira wake 

Daktari wa Simba SC akimtoa nje beki Hassan Hatibu baada ya kuumia kiasi cha kushindwa kuendelea na mchezo

Mkipalamoto amemlamba chenga Himid Mao, anaondoka...

Lakini shuti lake lilidakwa na Mwadini...lilikuwa bao la wazi sana alikosa

Gaudence Mwaikimba akipiga mpira kichwa ambao ulitoka nje sentimita chache 

Hatari langoni mwa Simba SC

Lakini salama...

Himid Mao akiwa ametoa mpira nje kupunguza kasi ya Haruna Chanongo wa Simba SC

Mwantika amezuia, anaanza kugeuka taratibu

Miraj Madenge akishangilia baada ya kuifungia Simba bao la pili

Kutoka kulia ni Hassan Khatibu na Rashid Ismail wakicheza na Miraj Madenge kumpongeza kwa kufunga bao la pili 

Mkipalamoto akitafuta mbinu za kumtoka Mwantika

Hapa ni wakati Azam ikiwa nyuma kwa 2-1, tazama sura ya kocha wa Azam, Muingereza Stewart Hall ilivyokuwa

Brian Umony akiwa benchi baada ya kutolewa 

Kipa wa Simba SC, William Mweta akigagaa mpira ukiwa nyavuni...ni baada ya mkwaju wa penalti wa Joackins Atudo kuipatia Azam bao la kusawazisha

Wachezaji wa Azam Seif Abdallah kulia na Humphrey Mieno kushoto wakiwa kwenye benchi baada ya kutolewa

Makocha wanne wa kigeni wa Azam wakiwapa mawaidha wachezaji wao kabla ya kuingia kumalizia dakika 30 za nyongeza

Kuna wakati ilibidi Stewart Hall aombe ushauri kwa mchezaji wake wa akiba, Luckson Kakolaki kushoto ambaye anamuambia cha kufanya, bila shaka ilikuwa ushauri mzuri na ndiyo maana timu ilishinda.

Shujaa wa Azam, Malikqa Ndeule akiwa amebebwa juu juu