Kikosi cha Azam Fc
Tusker Fc
FAINALI ya michuano ya kuwania Kombe la Mapinduzi
inatarajiwa kupigwa leo Zanzibar kwa mabingwa
watetezi, Azam FC kuwakabili mabingwa wa soka wa Kenya , Tusker katika Uwanja wa
Amaan.
Wakati Azam wakikata tiketi ya fainali kwa kuing’oa Simba
katika nusu fainali kwa penalti 5-4, Tusker imetoka kuitandika Miembeni mabao
2-0.
Akizungumza kwa simu kutoka Zanzibar , Kocha Msaidizi wa Azam, Kally
Ongara alisema wamejipanga vizuri kutetea ubingwa wao kwa mara nyingine huku
akisema mechi hiyo itakuwa ya ushindani mkubwa kutokana na umahiri wa wapinzani
wao.
“Itakuwa mechi yenye ushindani mkubwa, ni mechi
inayozikutanisha timu zilizofanya vizuri kuanzia hatua ya awali na ndiyo maana
zikafika fainali, hivyo licha ya uwezo kila moja itakuwa ikihitaji ubingwa.
“Tumejiweka vizuri kuhakikisha kombe linabaki nyumbani kwani
itakuwa aibu kombe hili liende nje ya mipaka yetu,” alisema Ongara aliyewahi
kukipiga Yanga.
Azam leo itawakosa nyota wake kadhaa wakiwemo waliopo timu
ya soka ya Tanzania, Taifa Stars ambayo jana ilicheza na Ethiopia mjini Addis
Ababa huku nyota kama Waziri Salum, Ibrahim Mwaipopo, Abdulhalim Humud, Abdi
Kassim, John Bocco, Kipre Tchetche na Jabir Aziz, wakiwa majeruhi na wengine
kutumikia kadi nyekundu.
Michuano hiyo ambayo ni mahususi kwa ajili ya kuadhimisha
Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12,
1964, ilianza kutimua vumbi Januari 2 ikishindanisha timu za Tusker, Miembeni,
Jamhuri ya Pemba , Simba, Azam FC, Coastal
Union na Mtibwa Sugar.
Licha ya kila timu kujipanga kutwaa ubingwa wa michuano hiyo,
filimbi ya mwisho ndio itasema kweli kama
kombe litabaki kwa Azam au kutwaliwa na timu kutoka nje kwa mara ya kwanza.
Comments
Post a Comment