AMIR MAFTAH NDIO BASI TENA SIMBA SC...NYOSO NDANI YA NYUMBA


LICHA ya beki Amir Maftah (Pichani) kuandika barua ya kuomba msamaha, inadaiwa klabu yake ya Simba haina mpango tena wakumrejesha kundini, imefahamika.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Maftah, beki mwingine wa timu hiyo aliyekuwa akitumikia adhabu ya kwenda kuongeza kiwango chake timu B, Juma Nyoso amerejeshwa kundini na jana aliungana na wenzake katika mazoezi yanayoendelea kwenye viwanja vya TCC Chang’ombe, Temeke jijini Dar es Salaam.
Maftah, alitakiwa kujieleza kutokana na kushindwa kujiunga na wenzake tangu kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom, bila ya sababu za msingi.
Akizungumza hivi karibuni, kiongozi mmoja wa Simba alisema, licha ya Maftah kubakiza miezi michache ya mkataba wake, hawana mpango wa kumrejesha kundini.
Kiongozi huyo alisema kwamba, wameamua kuachana na Maftah, kutokana na kukerwa na vitendo vyake vya utovu wa nidhamu, ambavyo amekuwa akivifanya kwa nyakati tofauti.
Alisema, kumrejesha Maftah ni sawa na kuruhusu kuendelea kuwepo kwa ‘virusi’ ndani ya klabu hiyo, ambavyo vitaweza kuleta madhara makubwa katika siku za usoni.
“Simba ya sasa ni nyingine kabisa, kwani hatuangalii majina wala uzoefu, kikubwa zaidi tunahitaji wachezaji wenye nidhamu, kinyume na hapo huwezi kuwa na nafasi ya kuicheza Simba,” aliongeza kiongozi huyo.
Mbali na kutojiunga na wachezaji wenzake alipohitajiwa kwa nyakati tofauti, Maftah pia anatuhumiwa kumtukana kiongozi mmoja wa juu wa Simba, kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, akimtuhumu kumbania fedha zake za usajili.
Maftah aliyesajiliwa Simba mwaka 2011 baada ya kutemwa Yanga, mkataba wake unatarajiwa kumalizika Mei mwaka huu, ambako kupitia barua yake hiyo ya kuomba msamaha, pia ameomba kupewa fedha zake za usajili sh milioni nne.
Katika hatua nyingine, beki Juma Nyoso, amerejeshwa kundini na kuungana na wenzake katika mazoezi ya kujiandaa na mchezo wao wa ligi dhidi ya JKT Ruvu utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Jumapili.
Nyoso ambaye alisimamishwa Oktoba mwaka jana pamoja na Haruna Moshi ‘Boban’, kutokana na utovu wa nidhamu na kiwango kushuka, kabla ya uongozi kumpa adhabu ya kukichezea kikosi cha pili cha timu hiyo.