CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA)
kinaendelea na maandalizi kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa chama hicho
utakaofanyika Desemba 21 na 22 mwaka huu Kiromo View Resort Hotel, Bagamoyo
mkoani Pwani.
Lakini bado kuna mwitikio mdogo wa wanachama wanaothibitisha
ushiriki wao, ambapo hadi kufikia leo saa tano asubuhi waliothibitisha ni 22
tu, hivyo tunasisitiza wengine wafanye hivyo haraka na tusikubali kufanya mambo
kwa mazoea na mwisho wa kuthibitisha ni Jumamosi Desemba 15, saa kumi alasiri na
watakaokwama kufanya hivyo watahesabika wamekosa sifa ya kushiriki mkutano.
Tunaomba wanachama wote ambao wanatarajia kuhudhuria mkutano
huo wathibitishe ushiriki wao kwa Katibu Mkuu wa TASWA kwa njia ya email:
mgosius@yahoo.com au taswatz@yahoo.com.
Kamati ya Utendaji ya TASWA inaendelea na juhudi za kutafuta
wadhamini kwa ajili ya Mkutano Mkuu, ambapo kiasi cha Sh. Milioni 20
kinahitajika kufanikisha mkutano ikiwa ni gharama mbalimbali ikiwemo chakula,
malazi, usafiri kwa wanachama wa Dar
es Salaam , pamoja na usafiri na malazi kwa wanachama
wanaotoka nje ya Dar es Salaam.
Tayari wadau watatu wamejitokeza kupiga jeki mkutano huo,
ambapo Alhamisi Desemba 13 saa tano asubuhi mgahawa wa City Sports Lounge
Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto atatangaza mdhamini mmoja ambaye tutakuwa
tumemalizana naye.
Kiasi cha fedha kinachohitajika ni kikubwa sana , hivyo bado jitihada zinaendelea
kutafuta wadhamini wengine kuhakikisha mkutano unakuwa wa mafanikio makubwa na
tunaomba wenye nia ya kushirikiana nasi wafanye
hivyo.
Licha ya wanachama pia tunatarajia katika mkutano huo pia
watakuwepo wadau mbalimbali wa TASWA wakiwemo waandishi wakongwe wa habari za
michezo ambao watapewa nafasi ya kuzungumza.
Wanachama wa TASWA watapata fursa ya kupokea na kujadili
Ripoti ya Utendaji ya chama, Mapato na Matumizi, maendeleo ya chama na masuala
mbalimbali yanayohusu waandishi wa habari za michezo kwa ujumla.
Pia kutakuwa na semina maalum itakayoendeshwa kwa washiriki
wa mkutano huo ili wawe na uelewa kuhusiana na ajenda ya kuinua kipato kwa
wanachama ambayo itajadiliwa kwenye mkutano huo.
Kamati ya Utendaji ya TASWA imekubaliana iwasaidie wanachama
wake waweze kujitegemea kwa kuanzisha Chama cha Akiba na Mikopo (SACCO’S),
lakini imeamua kwanza iwaite wataalamu wa vyama vya ushirika watoe elimu juu ya
jambo hilo na kukishakuwa na uelewa wa kutosha
suala hilo lipelekwe kama
ajenda kamili ya kuanzisha chama hicho kwenye Mkutano Mkuu.
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
10/12/2012
Comments
Post a Comment