VIGOGO SIMBA WATUA KAMPALA KUMALIZA MZIZI WA FITNA

MWENYEKITI wa klabu ya Simba Alhaj Ismail Aden Rage pamoja na mwenyekiti wa kamati ya Usajili Zakaria Hanspope wametua mjini Kampala, Uganda kwa ajili ya kushughulikia masuala mbalimbali ikiwemo kuzungumza na winga wao Mrisho Ngassa,ambaye inadaiwa kuwa ameuzwa na Azam katika klabu ya El Merreikh ya Sudan kwa dola za Kimarekani 50,000.
Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam zinaeleza kwamba, Rage na Hanspope watazungumza na Ngassa kuhusiana na hatua hiyo kutokana na ukweli kwamba bado ni mali ya Simba na iweje akubali kuuzwa bila ya uongozi wa Simba kushirikishwa.
Kama hiyo hitoshi, viongozi hao pia wanatarajiwa kufanya mazungumzo na kocha wa timu ya taifa ya Malawi, Mzambia Kinnah Phiri ili aweze kuja kurithi mikoba ya Mserbia Milovan Cirkovic ambapo Simba imeamua kuachana naye.
Aidha, taarifa zinaeleza kuwa, viongozi hao wamekwewnda na 'mkwanja' wa kutosha ambapo pia utatumika kumwagia, mshambuliaji wao wa Kimataifa Emmanuel Okwi ili aweze kuongeza mkataba wa kuichezea klabu hiyo.
Mpaka sasa Okwi ambaye yupo huko akiichezea timu yake kwenye michuano ya Chalenji inayoendelea nchini humo, amegoma kuongeza mkataba wake Simba mpaka apatiwe dola 40,000.