Baadhi ya vitu vya marehemu Hussein Mkieti ‘Sharo Milionea’
vilivyokamatwa baada ya msako mkali uliowashirikisha Polisi na wananchi wa
Kijiji Songa Kibaoni, Muheza (Picha na Bertha Mwambela,Tanga)
Mbaruku Yusuph na Bertha Mwambela, Muheza
VITU vilivyoporwa na watu wasiojuliana katika ajali ya msanii
mahiri wa filamu na muziki wa kizazi kipya nchini, Marehemu Hussein Mkieti ‘Sharo
Milionea’ eneo la Songa Kibaoni wilayani Muheza mkoani Tanga, vimesalimishwa na
wananchi wanaosadikiwa ni wezi.
Ajali hiyo ilitokea Jumatano iliyopita eneo hilo majira ya saa 2:30 nusu
usiku, baada ya gari alilokuwa akiliendesha msanii huyo, Toyota Harrier kuacha
barabara na kuingia porini lilikogonga mti kisha kupinduka na kumsababishia
mauti.
Msanii huyo alikuwa akitokea jijini Dar es Salaam kuelekea kijijini kwao Lusanga
Muheza kwa ajili wa kuwasalimia wazazi wake pamoja na kuwapelekea fedha za
matumizi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe, jana
alithibitisha kupatikana vitu hivyo, ambako alisema upatikanaji wake ulitokana
na msako mkali uliofanywa na uongozi wa serikali Muheza wakishirikiana na Jeshi
la Polisi wilayani humo.
Kamanda Massawe alisema, baada ya kutokea kwa tukio hilo , Jeshi la Polisi mkoani Tanga, liliweka mtego na
kutangaza kuinunua simu ya mkononi ya msanii huyo aina ya ‘blackberry’, ndipo
moja kati ya wanaodaiwa vibaka waliohusika kwenye tukio hilo , alipojitokeza na kuipeleka kwa ajili ya
kuiuza.
Alisema, wakati walipofika eneo ambalo walikubaliana,
walikabidhi simu hiyo kwa ajili ya kuikagua, lakini baadaye wezi hao walishtukia
mtego huo na kukimbia huku wakiiacha simu hiyo.
Aidha, Kamanda
Massawe alivitaja vitu ambavyo vimesalimishwa kwa jeshi hilo
kuwa ni simu ya mkononi aina ya blackberry, Betri la gari, tairi la akiba, radio
ya gari, begi ambalo lilikuwa na nguo za marehemu, saa ya mkononi na nguo
ambazo alikuwa amevuliwa na vibaka wa eneo hilo mara baada ya kutokea ajali hiyo.
Aliongeza kuwa, msako unaendelea na wamebaini baadhi ya
washukiwa wa uhalifu huo wamezikimbia nyumba zao kwa hofu ya kukamatwa.
Alisema, hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na Polisi
kuhusiana na tukio hilo la uporaji na uchunguzi wa kuwabaini waporaji ili
waweze kutiwa mbaroni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria unaendelea, huku akitoa
wito kwa wananchi kuacha kufanya vitendo vya uporaji pindi ajali zinapotokea
katika maeneo yao.
"Tupo kwenye uchunguzi mkali ili kuhakikisha tuwatia
mbaroni wale wote ambao waliohusika na kitendo cha kinyama alichofanyiwa msanii
huyo,” alisema Kamanda Massawe.
CHANZO:GAZETI TANZANIA DAIMA
Comments
Post a Comment