TULIZIDIWA -POULSEN


Na mwandishi maalumu,
Kampala
Kocha wa Timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amekiri kuwa kikosi chake kilizidiwa na Cranes ya Uganda katika nusu fainali ya mashindano ya Cecafa Challenge huku akisema licha ya maandalizi mazuri, Waganda walikuja na mbinu ya kuwakabili.
Poulsen aliyasema hayo jana  baada ya mchezo huo ambapo Stars, inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager ililala kwa kukubali kichapo cha mabao 3-0.
“Ukizingatia kuwa walikuwa katika uwanja wa nyumbani, waliwapa wachezaji wetu taabu sana na tulifanya makosa kuruhusu goli la haraka katika dakika ya kumi na moja hivi,” alisema.
Alisema kuelekea mwisho wa kipindi cha kwanza Stars ilijitahidi kuhakikisha hakuna bao lingine linaingia na walikuwa na matumaini kuwa mchezo ungebadilika katika kipindi cha pili.
“Hata hivyo tulifanya makosa tena kuwaruhusu waganda kupiga krosi na kuziunganisha na kupata goli tena na hapo wachezaji wa Uganda wakapata nguvu zaidi hasa ikizingatiwa mashabiki wao walikuwa wamejaa uwanjani wakishangilia,” alisema Poulsen.
Kocha huyo kutoka Denmark, alisema walikubali hali halisi kwani walicheza na timu yenye kiwango cha juu.
“Ila nataka kusisitiza tu kuwa hatujakata tamaa kwani vijana wamepata uzoefu mkubwa katika mashindano haya na itatusaidia kusonga mbele kwani tumejitahidi kufikia hatua za mwisho za mashindano ambayo yalikuwa magumu kwani timu zote zilikuwa zimejiandaa vizuri,” alisema.
Alisema kwa sasa wanajiandaa na mechi dhidi ya Zanzibar Jumamosi  ili kupata mshindi wa tatu wa mashindano hayo. “Huu nao utakuwa mchezo mgumu kwani tumeshaona namna Zanzibar wanacheza,” alisema.
“Tulianza mashindano vizuri na ombi langu tu sasa kwa wachezaji ni tumalize vizuri kama tulivyoanza angalau tuweze kupata nafasi ya tatu katika mashindano haya,” alisema.

Katika fainali, Kenya itamenyana na mwenyeji Uganda katika uwanja wa Mandela uliopo Nambole, Jijini Kampala.
Akizungumza kutoka Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager aliipongeza Stars kwa hatua iliyofikia katika mashindano ya Cecafa Challenge huku akisema sio mwisho wa safari kwani bado kuna mashindano mengine.

“Tunaamini vijana wamepata uzoefu mkubwa na sasa wana silaha ya kukabiliana na mashindano mengine mbele yao…hatua waliofikia ni kubwa tu na tunawaomba wasife moyo,” alisema huku akiwataka watanzania pia kuwa na subira kwani timu bado inaonesha matumaini.

Stars inatarajiwa kurejea nyumbani Jumapili hii baada y mashindano kumalizika ili kujiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Chipolopolo ya Zambia ambapo Kilimanjaro Premium Lager inatarajiwa kuizindua Taifa Stars rasmi kwa watanzania.

Comments