TFF YATAKA USHINDANI UHAI CUP


SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF) limezitaka timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za vilabu vya ligi kuu bara, kujiandaa vema kwa ajili ya michuano ya ‘Uhai Cup’ inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Desemba 12. 
Katibu Mkuu wa TFF Angetile Osiah amesema leo  kwamba michuano hiyo ni muhimu katika mustakabali mzima wa maendeleo ya soka hivyo vilabu vinapaswa kufanya maandalizi ya uhakika. 
Alisema bila vijana soka haliwezi kuendelea hivyo vilabu shiriki havinabudi kufanya maandalizi ya uhakika ili kuweza kuleta ushindani katika michuano hiyo. 
“Ni matumaini yangu vilabu vimeandaa timu na si kukusanya vikundi vya wachezaji na kuvileta kushiriki kwani tunahitaji timu iliyofunzwa na si kukusanya wachezaji na mwisho wa siku hakuna mafanikio yoyote,”alisema 
Angetile aliongeza kuwa ratiba ya michuano hiyo itajulikana rasmi kesho jumamosi  ambapo kutafanyika droo maalum kwenye ofisi za Shirikisho hilo. 
Timu zinazotarajiwa kushiriki ni pamoja na mabingwa watetezi Simba, Yanga, Azam, Coastal Union, Mgambo Shooting , Mtibwa Sugar, Polisi Dodoma, Kagera Sugar, African Lyon, Ruvu Shooting, JKT Ruvu, Tanzania Prisons, Oljoro JKT na Toto African.

Comments