SIMBA WAMUWEKA REHANI OKWI BAADA YA KUTAKA DOLA 40,000 ILI AMWAGE WINO


KUTOKANA na Klabu ya Simba kukabiliwa na ukata wa fedha, inaelekea kushindwa kumbakisha mshambuliaji wake wa kimataifa, Mganda Emmanuel Okwi ambaye anataka dau la dola 40,000 za Marekani kabla ya kusaini mkataba mpya, imefahamika.
Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi zinasema tayari Simba wameanza mazungumzo na Azam kwa lengo la kumuuza huko kwa kiasi cha fedha watakachoafikiana.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa hatua ya kutaka kumuuza Okwi kwa Azam ni kutokana na Simba kutokuwa na fedha za kumpa ili aweze kubaki katika kikosi cha timu hiyo kitakachocheza Ligi ya Mabingwa Afrika mapema mwakani.
“Kwa kifupi Okwi ametaka kiasi hicho cha fedha, kinyume na hapo hawezi kuongeza mkataba wa Simba katika mzunguko wa pili na michuano ya kimataifa,” alisema kiongozi mmoja wa timu hiyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Aliongeza kwamba kwa sasa wanaelekeza nguvu zao kwa ajili ya kumuuza nyota huyo ili wapate fedha kwa ajili ya usajili wa nyota wengine na kuwaongezea mikataba baadhi yao waliopo kweye kikosi cha timu hiyo.
Alisema tayari wameanza mazungumzo na Azam ya kumuuza Okwi na kudokeza kuwa mazungumzo ya awali yamekwenda vizuri kwani sasa wanasubiri ofa watakayoitoa wao Simba kuona kama wataimudu au la.
Juhudi za kutaka kumuuza Okwi zinakuja huku nyota huyo mahiri akibakisha miezi mitatu kwenye mkataba wake wa kuitumikia timu hiyo inayopigana kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Bara.
Mkakati wa Simba kumuuza nyota huyo umechukua kasi huku kukiwa na habari kuwa baadhi ya timu za Afrika na Ulaya zimeonesha nia ya kumtaka nyota huyo mahiri kwa upachikaji mabao, aliyeisaidia Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita.
 Okwi kwa sasa yupo nchini Uganda akiitumikia timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ inayoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji

Comments