SERIKALI YAFAGILIA UHURU MARATHON


Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imepongeza wazo la kuanzishwa mbio za Uhuru Marathon ambazo zitakuwa zikifanyika kila mwaka, lengo likiwa ni kudumisha umoja, amani na upendo miongoni mwa Watanzania na kuuenzi uhuru wetu. 
Pongezi hizo zilitolewa na Waziri wa habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara wakati wa uzinduzi wa mbio hizo katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya JB Belmont jijini Dar es Salaam juzi usiku. 
Dk. Mukangara alisema kuwa, kwa sasa kuna mbio nyingi za marathon hapa nchini, lakini hakuna ambaye alikuja na wazo zuri la kuanzisha mbio kama hizo za kuuenzi uhuru wetu na kudumisha amani nchini. 
“Nawapongeza waandaaji wa mbio hizi ambao ni vijana wa Kitanzania waliokuja na wazo hili zuri la kuanzisha mbio za uhuru. Tunazo mbio nyingi sana hapa nyumbani, lakini hatukuwa tumewaza kuanzisha mbio zinazolenga kuuenzi uhuru wetu na kudumisha amani yetu. 
“… Kwa niaba ya Serikali, napenda kusema wazi kuwa tumefurahishwa sana na wazo hili la kuanzisha mbio hizi za uhuru na nichukue fursa hii kuwaomba wadau na wapenda maendeleo ya michezo kuungana na taasisi hii kufanikisha mpango huu ili uweze kuwa na mafanikio. 
“Serikali bado itaendelea kuweka miongozo na mazingira rafiki ya kushirikiana na wadau wenye nia nzuri ya kuendeleza michezo nchini. Nina hakika waheshimiwa mawaziri, wabunge, viongozi mbalimbali wa Serikali, mashirika binafsi na viongozi wa dini wote watajitokeza kushiriki mbio hizi,” alisema. 
Awali Mkurugenzi wa Kampuni ya Intellectuals Communications, Innocent Melleck, walio waandaaji wa mbio hizo, alimuomba waziri afikishe ombi lao kwa Rais Jakaya Kikwete kuwa mlezi wa mbio hizo. 
Pia walimkabidhi Dk. Mukangara fulana maalumu ya Rais Kikwete pamoja na ya Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, kutokana na mchango wao maalumu kwa mbio hizo. 
“Mbali na hilo tunapenda kuweka milango wazi kwa taasisi, kampuni na watu mbalimbali kudhamini mbio hizo zenye malengo mazuri kwa Taifa,” alisema. 
Mbio hizo zinatarajiwa kuanza rasmi mwakani na zitakuwa zikifanyika kila Desemba 8, kwa ushirikiano mkubwa wa Berlin Marathon na London Marathon.