SERIKALI YAAHIDI KUUNGA MKONO MBIO ZA KILI MARATHON


Mkuu wa wilaya ya Moshi, Dk. Ibrahim Msengi akikata utepe kuzindua mbio za Kilimanjaro Marathon mkoani Kilimanjaro mwishoni mwa wiki. Kushoto kwake ni mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro Listone Metacha na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe (Picha: Executive Solutions)
SERIKALI mkoani Kilimanjaro, imesema itaendelea kuunga mkono mbio ndefu za Kilimanjaro Marathon, zitakazofanyika mkoani humo mwezi Machi mwakani kutokana na umuhimu wake katika kuutangaza mlima Kilimanjaro, Mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania kwa ujumla.
Ahadi hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa huo Leonidas Gama, wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo kwa mwaka 2013, uliofanyika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na  viongozi mbalimbali, wanamichezo na wakazi mbali mbali wa mji huo na Mikoa ya jirani.
“Mashindano ya kimataifa ya Kilimanjaro Marathon ni moja wapo ya matukio muhimu katika kalenda ya michezo hapa nchini na ambayo imekuwa ikiwavutia washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi hivyo hatuna budi sisi kama serikali kuungana na wadau wengine katika kuhakikisha yanaendela kuwepo”, alisema.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Ibrahim Msengi, Gama alitoa changamoto kwa wanariadha  na viongozi wa riadha hapa nchini kuhakikisha wanatayarisha timu ambayo itawezesha watanzania kushinda mbio hizo mwakani.  
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alitoa pongezi zake kwa wadhamini wakuu wa mbio  hizo Kilimanjaro Premium Lager pamoja na wadhamini wengine kwa kuendelea kuunnga mkono uwepo wa mashindano hayo kupitia udhamini mbalimbali.
Kwa upande wake meneja wa bia  ya Kilimanjaro Premium Lager ambao ndiyo wadhamini wakuu wa mashindano hayo George Kavishe, alisema watatoa motisha ya zawadi ya shilingi milioni 3 ya ziada kwa wanariadha wa kitanzania watakaoshinda mbio za 42 km Kilimanjaro Premium Lager Marathon. Hii ni kuwapa moyo Watanzania waweze kufanya vizuri katika mbio hii ambayo inafanyika hapa kwenye ardhi yao.
“Iwapo mwanariadha wa Tanzania awe wa kike au wa kiume atashinda mbio hizo Machi, mwakani, mbali na zawadi ya kwanza ya shilingi mioni tatu, ataongezewa milioni nyingine tatu”, alisema.
Alisema matokeo ya mbio zilizopita jana yaliibua changamoto kubwa kwa wanariadha wa Tanzania, viongozi wa riadha na wadhamini wenyewe na kwamba mwaka huu wadau mbalimbali wamejipanga kuhakikisha watanzania wanashika nafasi ya kwanza mwakani.
Kawishe aliendelea kusema kuwa Kilimanjaro premium lager itaendelea kudhamini mashindano  hayo muhimu ya kimataifa na ambayo alisema ymeiletea Tanzania heshima kubwa. Pia aliwashukuru wadhamini shirikishi Vodacom, GAPCO, Tanga Cement, CFAO Motors, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, Shoprite, New Arusha Hotel na Kilimanjaro Water kwa kuendelea kuziunga mkono mbio hizo.


Comments