MKUTANO MKUU WA TASWA KUFANYIKA DESEMBA 21 NA 22 MJINI BAGAMOYO


MKUTANO Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) utafanyika Desemba 21 na 22 mwaka huu Kiromo View Resort Hotel, Bagamoyo mkoani Pwani.

Mkutano huo unatarajiwa kushirikisha wanachama 100, na pia watakuwepo wadau mbalimbali wa TASWA wakiwemo waandishi wakongwe wa habari za michezo wambao watapewa nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo.

Wanachama wa TASWA watapata fursa ya kupokea na kujadili Ripoti ya Utendaji ya chama, Mapato na Matumizi, maendeleo ya chama na masuala mbalimbali yanayohusu waandishi wa habari za michezo kwa ujumla.

Pia kutakuwa na semina maalum itakayoendeshwa kwa washiriki wa mkutano huo ili wawe na uelewa kuhusiana na ajenda ya kuinua kipato kwa wanachama ambayo itajadiliwa kwenye mkutano huo.

Kamati ya Utendaji ya TASWA imekubaliana iwasaidie wanachama wake waweze kujitegemea kwa kuanzisha Chama cha Akiba na Mikopo (SACCO’S), lakini imeamua kwanza iwaite wataalamu wa vyama vya ushirika watoe elimu juu ya jambo hilo na kukishakuwa na uelewa wa kutosha suala hilo lipelekwe kama ajenda kamili ya kuanzisha chama hicho kwenye Mkutano Mkuu.

Nia yetu ni kuona tunapiga hatua za kimaendeleo na kuwafanya wanachama wetu wafurahie kujiunga na chama hiki na waweze kupata mikopo ya kuwasaidia katika masuala mbalimbali.

Tunawaomba wanachama wote ambao wanatarajia kuhudhuria mkutano huo wathibitishe ushiriki wao kwa Katibu Mkuu wa TASWA kwa njia ya email: mgosius@yahoo.com au taswatz@yahoo.com. Mwisho wa kuthibitisha ni Desemba 15, 2012 saa kumi alasiri ili maandalizi mengine yaendelee na uwepo wao katika mkutano uthaminike.

Wanachama ambao wanajua hawajalipa ada ni vyema wakafanya hivyo,  kwa kuwasiliana na Mhazini Mkuu wa TASWA, vinginevyo chama kitafanya utaratibu mwingine wa kuhakikisha ada zao zinapatikana siku ya mkutano.

TASWA inaendelea na mazungumzo na wadhamini mbalimbali na Jumatatu Desemba 10, 2012 saa tano asubuhi katika mgahawa wa City Sports Lounge Dar es Salaam itatangaza mdhamini wa mkutano huo.

Nawasilisha.

Amir Mhando

Comments