MKUTANO MKUU TASWA WAPIGWA KALENDA


KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), iliyokutana katikati ya wiki jijini Dar es Salaam imekubaliana na mapendekezo ya baadhi ya wanachama kuomba isogeze mbele kwa wiki moja Mkutano Mkuu wa chama hicho.
Awali mkutano huo ulipangwa kufanyika Desemba 21 na 22 mwaka huu Kiromo View Resort Hotel, Bagamoyo mkoani Pwani, hivyo sasa utafanyika Desemba 28 na 29 mahali hapo hapo.
Hatua hiyo ya kusogeza mbele inatokana na baadhi ya wanachama kuomba iwe hivyo kutokana na Jumamosi ya Desemba 22 kutakuwa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na ile ya Zambia ‘Chipolopolo’ kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa msingi huo tumekubaliana na hoja kwamba mchezo huo kwa kiasi fulani ungeathiri umakini wa wajumbe kwenye mkutano kwa namna moja au nyingine, hivyo kupunguza tija.
Tunaamini idadi kubwa ya wanachama waliothibitisha kushiriki ni ishara kwamba wengi wanataka kujumuika kwa asilimia kubwa katika kukijenga chama chao, hivyo hatuoni sababu ya kufanya mkutano kwa kukurupuka.
Hadi kufikia Desemba 15 ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya wanachama kuthibitisha ushiriki wa mkutano zaidi ya asilimia 95 ya wanachama walikuwa wamethibitisha kushiriki.
Kutokana na hali hiyo wote waliothibitisha ushiriki huo na ni hai watajulishwa kwa barua rasmi, ambazo zitaeleza utaratibu wa namna ya kufika Bagamoyo na mambo mengine muhimu yatakavyokuwa.Barua zitaanza kutoka wakati wowote kuanzia Jumatano ijayo baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kinachotarajiwa kufanyika siku hiyo.
Pia tayari TASWA imewaalika wadau mbalimbali wakiwemo wahariri wakongwe ambao wamethibitisha kushiriki kwenye mkutano huo wa aina yake.TASWA baada ya kupata udhamini wa Zantel  kwa ajili ya mkutano huo bado inaendelea na mazungumzo na wadhamini mbalimbali na inatarajia kuwatangaza wakati wowote mambo yatakavyokuwa mazuri. 
(B)         Pongezi
TASWA inawapongeza viongozi wapya wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) walioingia madarakani Desemba 8, mwaka huu mkoani Dodoma, ambapo Ghullam Rashid alichaguliwa tena kuwa Rais, huku Filbert Bayi akichaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu.
Tunaahidi kuendelea kushirikiana na uongozi wa TOC kama ilivyokuwa wakati uliopita na kuwatakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yao na tuna imani watafanya vyema.
(C)         Msiba:
Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya msiba wa mwandishi wa zamani wa habari za michezo, Amina Singo kilichotokea usiku wa kuamkia leo.
Tunaungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu kwani wakati wa uhai wake alikuwa mdau mkubwa wa TASWA wakati huo akiwa mtangazaji wa habari za michezo wa Redio Times FM, hivyo kifo chake ni pengo kubwa kwa tasnia ya uandishi wa habari hapa nchini.
Kwa mujibu wa marafiki za marehemu msiba upo Mbezi na mipango ya mazishi inaendelea. Tukipata taarifa zaidi tutajulishana.

Nawasilisha.

Amir Mhando
Katibu Mkuu
16/12/2012.

Comments