LAPF YAHAMASISHA WASANII KUJIUNGA NA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII


Wasanii nchini wametakiwa kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika mifumo ya hiari kwa lengo la kujiwekea akiba ya kuwasaidia katika masuala mbalimbali kwenye maisha baada ya kufikia hali ya kushindwa kufanya kazi.
Akiwasilisha mada ya umuhimu wa wasanii na wadau wa sanaa kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Afisa Utekelezaji  wa  Mfuko wa Pensheni  wa  LAPF, Emmanuel Maishaa amesema katika kipindi hiki ambacho Serikali imetoa uhuru kwa mifuko kusajili wanachama walio nje mifumo rasmi ya ajira ni vyema wasanii kutumia nafasi hiyo kujiunga na mifuko na kujiwekea akiba.
“Tunafahamu kwamba si rahisi pengine msanii kupata fedha kila mwisho wa mwezi, lakini kwa mfumo wetu LAPF tunatoa nafasi ya kuchangia kadri unavyopata. Nadhani na mifuko mingine inautaratibu wake lakini LAPF tumeliangalia hilo na kutoa nafasi nzuri zaidi ili hata msanii mwenye kipato cha chini kabisa aweze kumudu kuchangia,” alisema.
Amesema kwa kujiunga na mifuko ya jamii hasa LAPF wasanii wanaweza kupata faida nyingi ikiwa ni pamoja na kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na mifuko hiyo hivyo kujiwekea mazingira mazuri ya baadaye au ya kuwawesha kufanya mambo yao kwa urahisi baadaye.
“Msanii anaweza kujiunga na mfumo wa hiari ambapo baada ya mwaka mmoja LAPF inatoa nyongeza ya asilimia tano kwenye michango yake, na anaweza kujitoa wakati wowote baada ya kutimiza mwaka mmoja, katika mfumo huu kiwango cha chini cha kuchangiakwa mwezi ni shilingi 20,000/- ambapo msanii anaweza kulipa kiwango hicho kwa awamu na kwamba kuna nafasi ya kulipia kwa mkupuo kama amechelewa au kupitisha mwezi mmoja,” alisema

Comments