KOCHA MPYA SIMBA KUKISHUHUDIA KIKOSI CHAKE KIKIIVAA TUSKER FC JUMAMOSI


KOCHA mpya wa Simba Mfaransa Patrick Liewang anatarajia kukishuhudia kikosi ya timu hiyo jumamosi ya keshokutwa kitakapokwaana na mabingwa wa soka wa Kenya, Tusker Fc.
Mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki unatarajiwa kupigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam ambapo pia Simba itautumia kutambulisha nyota wake wapya iliyowasijili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Vodacom na michuano ya kimataifa.
Ofisa habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema leo kwamba, kocha huyo ambaye alikuwa awasili nchini leo imeshindikana baada ya kukosa nafasi kwenye ndege, hali itakayomfanya asubiri mpka jumamosi.
Alisema kocha huyo ambaye anakuja kurithi mikoba ya Mserbia Milovan Cirkovic, atakishuhudia kikosi cha Simba kikicheza mechi hiyo kabla ya kuendelea na taratibu nyingine ikiwemo kusaini mkataba wa kazi na baadaye kuanza kutumikia kibarua chake kipya.
Naye mratibu wa mchezo huo, George Wakuganda alisema kwamba maandalizi ya mchezo huo yamekamilika ambapo viingilio ni sh 15,000, 10,000, 7,000 na 5,000.
Tusker Fc jana ilikwaana na Yanga na kuitandika bao 1-0 mchezo ulipigwa kwenye uwanja wa Taifa.