KALUSHA BWALYA KUWAFUNDA WANASOKA WA BONGO


NGULI wa zamani wa soka nchini Zambia, Kalusha Bwalya (pichani)anatarajiwa kukutana na baadhi ya wachezaji wa Tanzania ili kuweza kuwapa ushauri wa jinsi gani ya kupata mafanikio katika medani hiyo. 
Bwalya ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha soka nchini Zambia (FAZ) anatarajiwa kuongoza msafara wa timu ya Taifa ya huko ‘Chipolopolo’ inayotarajiwa kutua nchini Desemba 18 tayari kuivaa Stars Desemba 22 kwenye Uwanja wa Taifa. 
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Angetile Osiah ameiambia Sports Lady kwamba kwamba anaamini Bwalya atakapokutana na wachezaji hao wataweza kupata hamasa ya kutosha katika kufikia mafanikio yake. 
Alisema TFF inafarijika kuona Tanzania inapata wasaa wa kutembelewa na wanasoka nguli kwa siku za hivi karibuni ambapo mwezi uliopita alikuja nyota wa kimataifa wa Ghana, Abed Pele. 
Osiah aliongeza kuwa ujio wa Chipolopolo umefanikishwa na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Grace Mujuna ambapo timu hiyo ityakuja na nyota wake wote wanaocheza soka la kulipwa katika nchi mbalimbali. 
Aliongeza kuwa kikosi cha Stars kinatarajiwa kuingia kambini mara baada ya kurejea nchini kutoka Uganda ambapo kinashiriki michuano ya Chalenji inayofikia tamati leo.