FAINALI KAWAMBWA CUP KUPIGWA KESHO VIWANJA VYA MWANAKELENGE


WAZIRI, DK.SHUKURU KAWAMBWA
FAINALI za mashindano ya kombe la mbunge wa Bagamoyo, Dk Shukuru Kawambwa ambaye pia ni Waziri  wa Elimu na Mafunzo ‘Kawambwa Cup’ zinatarajiwa kupigwa lkesho kwenye uwanja wa Mwanakelenge kwa kuzikutanisha timu za Mataya Fc na Beach Boys Fc, ambapo mshindi ataondoka na kombe pamoja na kitita cha sh.400,000. 
Timu hizo zilitinga faianli hiyo hiyo baada ya Mataya kuichapa Chaulu Fc mabao 3-1, huku Beach Boys iliwafunga Matimbwa Fc mabao 2-0 katika mechi za nusu fainali zilizopigwa juzi. 
Mratibu wa mashindano hayo, Masau Bwire alisema jana kwamba maandalizi ya fanali hizo yamekamilika ambapo pamoja na zawadi hizo, bingwa huyo pia atazawadiwa seti mbili za jezi, mipira miwili na seti moja ya vizuia ugoko. 
Alisema, mshindi wa pili atazawadiwa seti mbili za jezi, mipira miwili, seti moja ya vizuia ugoko, na fedha taslimu sh 200,000, huku mshindi wa tatu atapata jezi seti moja, mpira mmoja, seti moja ya vizuia ugoko na fedha taslimu sh 100,000, huku mwamuzi bora, kipa bora na  mfungaji bora kila mmoja atazawadiwa sh 50,000. 
Bwire aliongeza kuwa mgeni rasmi katika fainali hizo anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na MIchezo Dk Fenella Mukangara, huku pia Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodger Tenga atahudhuria fainali hizo na uongozi wa Chama cha soka mkoani Pwani (COREFA), pia utahudhuria.