DIAMOND AAMUA KURUDI DARASANI


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond Platinumz' ameamua kwenda shule kuongeza elimu kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kisanii na kimaisha, ili kuongeza ufanisi zaidi wa kazi zake.
Akizungumza katika kipindi cha Friday Night Live kinachorushwa hewani na televisheni ya East Africa (EATV) wiki iliyopita, msanii huyo alisema kwa sasa anasoma lugha ya Kiingereza, ujasiriamali pamoja na utawala katika chuo kimoja jijini Dar es Salaam.
“Nimeamua kusoma kwa lengo la kuziongoza vema shughuli zangu, tena kwa ufasaha hali ambayo itafanya kuwa tofauti katika kazi zangu,” alifichua Diamond katika mahojiano yake na mtangazaji Sam Misago.
Aliongeza: “Kwa maana somo la ‘management’ litanisaidia kuziweka sawa kazi zangu kitu ambacho kitanifanya kupata mafanikio zaidi.”
Msanii huyo anayetamba na wimbo wake mpya unaofanya vizuri kwenye vituo vya televisheni na redio. ‘Nataka Kulewa’, alishawahi kutamba pia na nyimbo kama vile ‘Mbagala’, ‘Nitarejea’, ‘Nimpende Nani’, ‘Lala Salama’ na nyinginezo.