YANGA SC KUZILETA TIMU KUBWA BARANI AFRIKA


MABINGWA wa kombe la Kagame, Yanga wanatarajiwa kuzileta nchini timu kubwa mbili kutoka moja ya nchi za Afrika ambazo zitacheza mechi ya kirafiki na timu yao na timu nyingine hapa nchini. 
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Binkleb (pichani) ameiambia Sports Lady hivi karibuni kwamba, wameamua kuzialika timu hizo ili kuja kuipa makali timu yao ambayo itakuwa katika maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi kuu bara na michuano ya Kagame. 
Alisema tayari wameshatuma maombi kwa timu kadhaa ambapo bado hazijatoa majibu kama zimekubali mwaliko huo au la, hivyo wataziweka wazi pindi zitakapothibitisha. 
Binkleb aliongeza kuwa kwa sasa hawawezi kuzitangaza timu nwalizozialika wakihofia kuchanganya mambo ikiwemo kuingiliana na mawakala katika suala hilo
Tayari, uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake Yussuf Manji umetangaza kuipeleka timu hiyo nchini Uturuki mwezi Desemba kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu na michuano ya Kagame. 
Katika hatua nyingine, Binkleb alisema hawana mpango wa kuacha mchezaji katika timu hiyo,zaidi watakachokifanya ni kuwapeleka kwa mkopo katika baadhi ya timu wachezaji ambao wanaona wameshuka viwango. 
“Suala la kujua nani atatolewa kwa mkopo lipo kwa kocha mkuu na sisi kama viongozi ndio tutaangalia ni wapi ambapo atahitajika kupelekwa,”alisema Binkleb