YANGA KUJENGA UWANJA UTAKAOBEBA MASHABIKI 40,000


KLABU ya Yanga imesaini makubaliano ya awali na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Kaunda.
Makubaliano hayo ya awali yalifikiwa na Mwenyekiti wa Yanga Yusuf Manji na Meneja Mkuu wa Kampuni hiyi David Zhang kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo kwenye makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga jana.
Ujenzi wa Uwanja huo utakaotumika kwa ajili ya mechi mbalimbali za timu hiyo utaanza Juni mwakani na utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuingiza kati ya watazamaji 30000 na 40000.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa makunaliano hayo jana Mwenyekiti wa Yanga Yusuf Manji alisema wanayo furaha kubwa kuanza safari ya ujenzi wa uwanja wao na ujenzi huo hautakuwa mwisho wa mipango yao ya kuifanya klabu hiyo kujitegemea kiuchumi.
“Lengo ni kuifanya Yanga ijitegemee kiuchumi, wote tumeona makato makubwa ya TFF, lakini tukiwa na vitega uchumi vyetu tutaifanya Yanga ijitegemee na kuepukana na makato hayo.”alisema Manji.
Alisema kwenye mipango yao ya kuitegemeza kiuchumi klabu yao lipo pia jingo lao la mtaa wa Mafia lakini wameona ni bora kuanza kujenga uwanja sehemu ambayo ina historia kubwa ya klabu ya Yanga na Tanzania kwa ujumla.
“Lipo pia jengo la mtaa wa Mafia nalo ni sehemu ya mipango yetu lakini tumeona tuanze na huku nyumbani sehemu ambayo ina historia ndefu na klabu ya Yanga na Tanzania kwa ujumla.”alisema Manji.
Manji alisema chini ya uongozi wake wamedhamiria kufanya kitu kitakachoacha historia hapa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla hasa ukichukulia ukweli ya kwamba Yanga ndio timu ya kwanza kwenye ukanda huu kumiliki uwanja wake.
Alisema ujenzi wa uwanja sio jukumu la uongozi wa klabu hiyo pekee bali ni jukumu la kila mwanachama na shabiki wa klabu ya Yanga, hivyo wanaomba ushirikiano wa hali na mali kutoka kwa mashabiki na wanachama wao kufanikisha ujenzi huo wa uwanja.
Manji alisema Jumatatu kampuni hiyo ya ujenzi kutoka China ambayo ndiyo iliyojenga Uwanja wa Taifa itachukua vipimo kwenye Uwanja wa Kaunda na Uongozi wa Yanga kuliwasilisha suala la ujenzi huo kwenye Mkutano Mkuu wa Wanachama wa klabu hiyo Desemba 8.
Alisema baadhi ya fedha kwa ajili ya uwanja huo wa kisasa watakapo benki na gharama nyingine zitatokana na michango ya wanachama baada ya kuwa wamepata gharama nzima za ujenzi za uwanja huo.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Beijing Cobnstruction Engineering Group alisema wanafurahia kufikia makubaliano ya awali ya ujenzi wa uwanja na klabu ya Yanga.
Alisema wao ndio walijenga Uwanja wa Taifa na viwango vya ujenzi vya uwanja huo vilisifiwa na timu ya taifa ya Brazil iliyokuja kucheza mechi ya kirafiki na Tanzania mwaka 2010 ikiwa njiani kuelekea Afrika Kusini ambako fainali za kombe la Dunia zilifanyika.

Comments