WATANZANIA WATINGA KAMPALA, WAIPA STARS USHINDI.

Na mwandishi wetu,
Kampala
Watanzania zaidi ya 120 ambao ni Mashabiki wa timu ya Tanzania bara,Kilimanjaro Stars walijitokeza Jijini Kampala na kuishangilia timu yaokwa staili ya aina yake na kuisababisha Stars kuibuka na ushindi katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Sudan katika michuano ya CECAFA
Challenge 2012.
Watanzania hao walitokea Mkoa wa Kagera huku akiongozwa na Mwenyekiti wa Bukoba Veterans, Ernest Nyabo.
Mashabiki hao walileta hamasa ya aina yake kwa wachezaji wa Stars,inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, kwani wachezaji walijituma na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
“Tuna mapenzi na timu yetu ndio maana tumeacha shughuli zetu na kupanda mabasi kuja huku Kampala kuiona timu yetu ikicheza na kuja kwetu kumezaa matunda kwani vijana wamecheza vizuri na kuibuka na ushindi,” alisema Bw Nyabo.
“Tumependa sana ushirikiano uliopo kati ya Mrisho Ngassa na John Bocco kwani imezaa matunda” alisema mwenyekiti huyo.
Walisema endapo Stars itasonga mbele zaidi mashabiki wengi zaidi watafunga safari kuja Kampala ili kuipa timu nguvu. 

“Tunachoomba tu ni wachezaji pia wawe karibu na sisi…wakifunga waje upande wetu tushangilie pamoja,” alisema.

Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, inayodhamini Kilimanjaro Stars, George Kavishe, aliipongeza timu hiyo kwa kuanza vizuri na kuwaomba wachezaji wasibweteke kwani wazidi kutia bidii ili washinde mechi zote zilizobaki na kutinga fainali.

"Tuna imani nao na tunasubiri walilete nyumbani ili tusherekee pamoja, tutazidi kuwapa sapoti kama wadhamini wao watupe ushindi tu," alisema.

Baadhi ya mashabiki waliokuwa wakifuatilia mchezo hup kupitia Super Sport walisema walifurahishwa na kiwango kilichooneshwa na Stars na wako tayari pia kufunga safari kutoka Dar es Salaam na mikoa mingine ili kuishangilia timu yao.
Baada ya ushindi huu Tanzania iko katika nafasi ya pili katika kundi B ikiwa na pointi 3 huku Burundi ikiongoza kwa wingi wa mabao kwani iliifunga Somalia mabao 5-1. Sudan inashika mkia ikiwa bila pointi wala bao.
Stars inakabiliwa na kibarua kigumu Jumatano kuikabili Burundi na baadaye Somalia Disemba 1ikiwa ni mechi ya mwisho katika hatua ya makundi.
Kocha wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amesema ana imani na wachezaji wake kwani wengi ni vijana na tayari wameonesha kuwa wana ari ya kushinda.
Alisema anasikitika kuwakosa washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kwani wangeongeza nguvu kwenye kikosi chake.
“Nasikitika kuwakosa lakini kama kocha nitawatumia wachezaji waliopo ila nina uhakika TFF wanalifuatilia suala hili ili wachezaji hawa waungane nasi,” alisema.
Stars iliendelea na mazoezi katika viwanja vya Chuo Kikuu Makerere huku Nahodha wake Juma Kaseja akiwaomba watanzania kuwapa moyo wachezaji kwani mashindano ni magumu lakini watapambana ili waweze kutwaa ubingwa.
“Siku za nyuma wachezaji wa timu ya Taifa wamekuwa wakizomewa sana nawaomba watanzania wawape wachezaji moyo ili tuweze kushinda,” alisema.

Comments