STARS YAILAZA HARAMBEE KIRUMBA

Wachezaji Stars (Picha ya Maktaba ya BIN ZUBEIRY)


Na Prince Akbar
TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeibwaga Kenya, Harambee Stars bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza jioni hii katika mchezo wa kirafiki ulio katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Hadi mapumziko, Stars ilikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na beki Aggrey Morris katika dakika ya nne, baada ya kupanda kusaidia mashambulizi.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa anayetambuliwa na FIFA, Oden Mbaga, Kenya walitawala dakika 10 za mwanzo, lakini baada ya hapo Stars wakafunguka nao na kuanza kula nao sahani moja na Harambee Stars.
Kipindi cha pili, Kenya walianza na mabadiliko kocha Henri Michel akiwapumzisha James Situma, Jerry Santo na Wesley Kemboi na kuwaingiza Christopher Wekesa, Anthony Akumu na Timbe Ayoub.
Pamoja na mabadiliko hayo, mambo yaliendelea kuwa magumu kwa Harambee Stars, kwani wenyeji waliendelea kucheza kwa makini, wakishambulia na kujilinda zaidi.
Kocha wa Stars naye, Mdemnark, Kim Poulsen aliwatoa Amir Maftah, Salum Abubakar, Mwinyi Kazimoto, Mbwana Samatta, Mrisho Ngassa na Thomas Ulimwengu na kuwaingiza Nassor Masoud ‘Chollo’, Amri Kiemba, Simon Msuva, John Bocco ‘Adebayor’, Shaaban Nditi  na Issa Rashid.  
Katika mchezo huo, mshambuliaji wa Kenya anayechezea AJ Auxerre ya Ufaransa alifichwa kabisa na mabeki wa Stars.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Harambee, Mfaransa Michel alionyesha kukerwa na matokeo hayo na kusema timu yake haikucheza vizuri, wakati Polusen, amefurahia ushindi huo akisema timu yake haijacheza kwa miezi miwili na baada ya siku mbili za mazoezi wameifunga Kenya.  
Taifa Stars; Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Amir Maftah/Nassor Masoud ‘Chollo’ dk70, Aggrey Morris, Kevin Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakar/Amri Kiemba dk69, Mwinyi Kazimoto/Simon Msuva dk69, Mbwana Samatta/John Bocco dk 84, Mrisho Ngassa/Shaaban Nditi dk72 na Thomas Ulimwengu/Issa Rashid dk 89.  
Harambee Stars; Frederick Onyango, Brian Mandela, Eugene Asike, James Situma/Christopher Wekesa dk 46, Edwin Wafula, Jerry Santo/Anthony Akumu dk 46, Peter Opiyo/Charles Okwemba dk 67, Patrick Obuya, Patrick Osaika/Mulienge Ndeto dk 73, Dennis Oliech na Wesley Kemboi/Timbe Ayoub dk 46.

Comments