STARS KUINGIA KAMBINI BAADA YA CHALENJI


Timu ya Taifa (Taifa Stars) inatarajia kuingia kambini baada ya kumalizika michuano ya Kombe la Chalenji inayofanyika Uwanja wa Taifa wa Mandela ulioko Namboole jijini Kampala, Uganda. Michuano hiyo iliyoanza Novemba 24 mwaka huu itamalizika Desemba 8 mwaka huu. 
Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa timu hiyo Kim Poulsen, Stars itaingia kambini kujiandaa kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya mabingwa wa Afrika, Zambia (Chipolopolo) itakayochezwa Desemba 23 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Baada ya pambano dhidi ya Chipolopolo, wachezaji watapata mapumziko ya wiki mbili kabla ya kuingia tena kambini Januari 6 hadi 20 mwakani kwa ajili ya mechi nyingine za kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco. 
Kim anatarajia kuongeza kipa mmoja kwenye kikosi chake ili kuwasaidia nahodha Juma Kaseja na Deogratias Munishi pamoja na chipukizi kadhaa kutoka timu za Taifa za vijana za Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys. 
Vilevile Kim anafuatilia wachezaji wengine kwenye timu ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) ambayo pia inashiriki michuano ya Kombe la Chalenji ikiwa katika kundi C pamoja na timu za Eritrea, Malawi na Rwanda.

Comments