SIMBA YAMPELEKA NYOSO COASTAL UNION

                                                                       Juma Nyoso
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam inakusudia kumtoa kwa mkopo beki wake Juma Nyoso kwa Coastal Union ya Tanga ‘Wagosi wa Kaya’, imefahamika.
Nyoso alishushwa hadi kikosi B cha Wekundu hao wa Msimbazi kwa madai ya kushuka kiwango, sambamba na kiungo Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye alisimamishwa kutokana na utovu wa nidhamu kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu bara.
Kiongozi mmoja wa Simba ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema jana kwamba, wameamua kumpeleka Nyoso Coastal kutokana na bado ana mkataba wa kuichezea Simba, lakini kama si hivyo angekwenda na maji.
Alisema, uongozi umefikia hatua ya kumuondoa kundini Nyoso, kutokana na ukweli kwamba, nidhamu mbovu aliyonayo inaweza kuleta athari kwa wachezaji wengine na hasa vijana.
Kuhusiana na Boban, alisema, suala lake bado lipo mezani kutokana na ukweli kwamba, nyota huyo ni muhimu ndani ya klabu hiyo, lakini kasoro ndogondogo tu ndizo zinamharibia.
Alisema, tayari wachezaji hao wamepewa barua za kujieleza kuhusiana na makosa yao na Kamati ya Utendaji ya Simba inatarajiwa kukutana ndani ya siku mbili kwa ajili ya kutoa uamuzi rasmi juu yao.