RAGE AWAPOTEZEA WANACHAMA WALIOJIORODHESHA KUMNG'OA


MWENYEKITI wa klabu ya Simba Alhaj Ismail Aden Rage amesema kwamba uongozi umebaini kwamba wengi wa wanachama wa tawi la Mpira Pesa waliojiorodhesha ili kushinikiza kufanyika  kwa mkutano wa dharura wa klabuu hiyo si hao. 
Hatua hiyo inafuatia wanachama hao kufanya maadhimio ya kujiorodhesha ili kufikisha akidi itakayotimiza mashaerti ya kufanyika kwa mkutano ili kuwaonmdoa madarakani viongozi wa sasa kwa madai ya kushindwa kuongoza. 
Rage amesema pamoja na  kubaini hilo, pia uongozi umegundua kwamba majina  ya wanachama hao yamenakiliwa katika leja ya wanachama ambayo ilipotea mikononi mwa kiongozi mmoja wa zamani. 
Alisema uongozi unaheshimu jitihada zinazofanywa na wanachama hao na kuzifanyia kazi, lakini hauwezi kutekeleza vitu ambavyo havikidhi vigezo vilivyopo katika katiba ya klabu hiyo.
 Rage alisema, katiba ya sasa ya Simba haiwatambui wanachama waliopo kwenye leja, badala yake inawatambua wale waliosajiliwa katika kompyuta.
 “Pamoja na wanachama hao kunakiliwa katika leja,tumebaini hata saini zilizowekwa ni za kughushi na tukifanya uchunguzi hasa tutabaini ni wengi tu hawana sifa,  kitu ambacho kinakwenda kinyume na katiba ya Simba,”alisema Rage
 Rage aliongeza kuwa, wanaamini mchakato huo unafanywa na baadhi ya watu wanaotaka kuleta chokochoko ndani ya klabu hiyo kitu ambacho ni kigumu kukitimiza kwa vile uongozi upo imara na unafuata katiba ya klabu hiyo.
 “Hatuwezi kujiuzuilu kwa ajili ya shinikizo la watu ambao tunafahamu wanatumika, sisi tunaongoza kwa kufuata katiba na tutachukua uamuzi kwa mujibu wa katiba pindi inapostahili,”alisema
 Aidha, Rage aliongeza kwamba uongozi wa klabu hiyo ulitarajiwa kukutana jioni ya jana kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mwenendo mbaya wa timu hiyo katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Vodacom uliomalizika wiki iliyopita na Simba kushika nafasi ya tatu.
 Hivi karibuni baadhi ya wanachama waliutakla uongozsi wa Simba chini ya Rage kuachia ngazi baada ya timu hiyo ambayo ilikuwa ikiongoza ligi kwa kipindi kirefu kupoteza mwelekeo baada ya kupoteza michezo yake.