POULSEN BADOI NA MATUMAINI MAKUBWA NA KILI STARS


Na Mwandishi wetu,
Kampala
Kocha wa Timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen  amesema mechi ya kesho (Jumamosi) dhidi ya Somalia katika michuano ya Cecafa Challenge yanayoendelea Jijini Kampala, ni ya kufa na kupona na kikosi chake kiko tayari kukamilisha kazi.
Kocha huyo aliyasema hayo wakati Stars, inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanajro Premium Lager, ikifanya mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo wake na Somalia ili kukamilisha michezo ya Kundi B inayojumuisha Burundi, Tanzania, Somalia na Sudan.
“Mechi hii ni sawa na kuwa na risasi moja na risasi hii unatakiwa kuitumia vizuri..ndio mtihani tunaokabiliwa nao katika mechi hii maana lazima tushinde ili tusinonge mbele katika mashindano haya,” alisema n akikosi chake kitapambana hadi dakika ya mwisho.
Alisema ana imani na kikosi chake kwani wachezaji wote wana ari ya ushindi na kuendelea na mashindano kwani wameshaonesha kiwango kikubwa katika mechi mbili zilizopita huku Stars ikishinda mechi moja shidi ya Sudan na kufungwa nyingine na Burundi.
“Katika mechi hii hakuna mchezo na nimeshawaambia wachezaji kabisa maana hapa ukifungwa unaondoka,” alisema.
Kocha Poulsen pia alisema amefarajika kurejea kwa mchezaji Shomari kapombe ambaye alijeruhiwa katika mechi dhidi ya Burundi juzi.
Kwa mujibu wa daktari wa timu, Dk Mwanandi Mwankemwa, mchezaji Mwinyi Kazimoto hataweza kucheza kwa kuwa bado anaendelea kupata nafuu kwa hivyo wamemshauri kocha ampumzishe katika mechi hii na baadaye Stars ikifuzu kucheza mechi zijazo.
Meneja wa Bia ya Kilimanajro Premium Lager, George Kavishe alisema mechi hii ni muhimu kwa Stars na kuwaomba watanzania wanaoishi Kampala kujitokeza kwa wingi kuishangilia.
“Vijana hawa wanahitaji sapoti kutoka kwa wadau wote  hasa katika mechi hii ya kesho itakayoamua kama Tanzania itafuzuu kuendelea au la….sisi tukiwa wadhamini wa timu tunafuatilia kwa karibu na tunawaomba Tanzania waishangilie na kuipa moyo timu yao,” alisema.

Kikosi kinachotarajiwa kuanza katika mchezo huu dhidi ya Somalia ni Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Issa Rashid, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Amri Kiemba, John Bocco, Shaban Nditi na Salum Abubakary.

Mchezaji Amir Maftah ameachwa maana ana kadi mbili za njano.

Comments