POULSEN ASEMA KASI ZAIDI ITAWAPA USHINDI DHIDI YA BURUNDI

Na mwandishi wetu,
Kampala

Kocha wa timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amesema ili vijana wake waweze kuibana Burundi katika michuano ya CECAFA Challenge Jumatano, ni lazima wacheze kwa kasi na pasi za haraka.
Aliyasema hayo baada ya mazoezi yaliyofanyika katika uwanja wa Mutesa II unaomilikiwa na klabu ya Express ya Uganda.
“Lazima tucheze kwa kasi kubwa sana tena kushinda ule mchezo na Sudan Jumapili kwani Burundi ni timu nzuri lakini tutawabana.”
Alisema ana imani kubwa na safu ya ulinzi kwani walifanya kazi nzuri katika mechi iliyopita na kwa mechi dhidi ya Burundi itabidi jitihada zaidi ifanyike ili wasifungwe.
“Tukiifunga Burundi basi tutajiwekea mazingira mazuri sana ya kutinga
robo fainali na itawapa vijana morali sana,” alisema Poulsen.
Wakati Stars inamenyana na Burundi katika kundi B, Somalia itacheza na Sudan ambazo zote zilipoteza mchezo wa kwanza.
Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe ambaye bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager inaidhamini Stars, aliwasihi watanzania kuifuatilia timu ikicheza hata kwa kupitia runinga na kuwapa vijana morali.
Aliwataka watanzania hasa wanoishi Uganda kujitokeza kwa wingi kushangilia timu yao ili iendelee kushinda.
“Sisi kama wadhamini tunafarijika kuidhamini timu
inayoshinda…wamecheza vizuri katika mechi za kirafiki na sasa tunaona muendelezo huu wa ushindi hata huko kampala.
Aliwaomba Watanzania pia wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu ya Taifa, Taifa Stars itakapocheza na Zambia  Disemba 23 katika Uwanja wa Taifa. 
Kilimanjaro Premium Lager itatumia mechi hiyo kuizindua timu kwa Watanzania.