NINA IMANI NA KIKOSI CHANGU-POULSEN

Kocha wa Timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amesema ana imani na timu yake itakayotupa karata ya kwanza kesho dhidi ya Sudan katika mashindano ya CECAFA Challenge.
Alisema suala la wachezaji  Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kutofika mpaka sasa halimtatizi kwa kuwa ameiandaa timu vizuri na atawatumia wachezaji waliopo.
 “Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaweza wasicheze katika mechi ya kesho kwa sababu hawajafika lakini mimi nikiwa kocha nimejiandaa vizuri na nina imani na wachezaji waliopo,” alisema.
“Nina imani TFF wanafuatilia suala hili na wachezaji hawa watajiunga na wenzao hivi karibuni lakini hii haituzuii kufanya vizuri kwani tumejiandaa vizuri,” alisema.
Kuhusu wachezaji kama Aggrey Morris, Mohamed Nassoro na Mwadini Ali kutoka Zanzibar kujiunga na wenzao kuichezea Zanzibar Heroes, Poulsen alisema pengo lao halitampa tatizo kwa kuwa ni changamoto.
“Timu hii ambayo inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kwa sasa ina wachezaji wengi chipukizi kwa hivyo huu ndio muda wa kuwapima vizuri kwani kwani  haya ni mashindano makubwa,” alisema.
Alisema wachezaji wote wana hali nzuri na wana ari ya kushinda mechi yao ya kwanza  dhidi ya Sudan ambazi zimo katika Kundi B pamoja na Burundi na Somalia ambazo zitacheza leo pia.
Timu za kundi A zilitarajiwa kucheza jana ambazo ni Kenya dhidi ya Uganda na Ethiopia dhidi ya Sudan Kusini.
Kundi C inajumuisha Zanzibar na Eritrea na Rwanda dhidi ya Malawi.

Comments