MSIGWA CUP KUANZA NOV.26


Mch.Peter Msigwa

Na Peter Mwenda

TIMU 28 za soka kutoka sehemu mbalimbali za Iringa mjini zimethibitisha kushiriki mashindano ya Kombe la Msigwa linalotarajia kuanza Novemba 26 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,Mratibu wa Kombe hilo, Abu Changawa Majeki alisema mashindano hayo yamegawanywa katika makundi matatu.

Alisema kundi la kwanza litacheza katika uwanja wa Ruaha, Kundi la pili litakuwa uwanja wa Mlandege na wengine watapambana uwanja wa Kihesa.

Mratibu huyo alisema mshindi wa kwanza atapata sh. mil. 1, mshindi wa pili sh.700,000 na mshindi wa tatu atazawadiwa sh. 500,000.

Alizitaja timu shiriki kuwa ni Bodaboda FC, Tax FC, maselemara FC, Isakalilo FC, Galilaya FC, Mivinjeni,Itamba,Lugalo,Magereza S.C, Mawelewela FC,Kwakilosa SC,Mwandege SC, Sengo FC,Jamaika FC.

Nyingine ni Nduli FC, Usalama (Polisi) FC,Mtivila SC, Doni FC, Kigonzile FC, Ngongo SC, Mwangata SC, Ruaha Shooting SC, Uronge SC, Magari Mabovu SC, Magorofani FC,Mshindo SC, Ilala SC na Kihesa Kilolo FC.

Mratibu huyo alisema mashindano hayo yatakayodhaminiwa na Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa wa CHADEMA, yatagharimu sh. mil. 18.5 kwa ajili ya kununua jezi kwa timu zote shiriki, zawadi na gharama nyingine.