STARS YALALA KWA BURUNDI


Mshambuliaji wa Tanzania John Bocco akichezewa kindava na mabeki wa Burundi mbele ya refa Ronnie Kalema wa Uganda.


Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
BAO pekee la mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Suleiman Ndikumana dakika ya 52, leo limeizamisha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars katika mchezo wa Kundi B, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge Uwanja wa Mandela, Namboole, usiku huu.  
Nahodha huyo wa Burundi, anayechezea Inter Stars ya nyumbani kwao kwa sasa, alifunga bao hilo kwa penalti, baada ya yeye mwenyewe kuangushwa kwenye eneo la hatari na Shomary Kapombe.
Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na Burundi walifanya mashambulizi mawili ya hatari zaidi, lakini sifa zimuendee ‘TZ One’, Juma Kaseja aliyeokoa hatari hizo.
Stars hawakucheza soka yao ya chini kutokana na hali mbaya ya Uwanja, kujaa matope, kuwa wenye kuteleza kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kutwa nzima ya leo.
Kipindi cha pili Stars walijitahidi kutaka kusawazisha mabao hilo, lakini bahati haikuwa yao na zaidi waliishia kukosa mabao mawili ya wazi.
Kwa matokeo hayo, Burundi imeendelea kuongoza Kundi A, kwa pointi zao sita, mabao sita ya kufunga na moja la kufungwa, wakati Bara inabaki nafasi ya pili kwa pointi zake tatu, Sudan ya tatu ikiwa na pointi tatu na Somalia yenye pointi moja inashika mkia.
Kikosi cha  Tanzania Bara leo kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe/Issa Rashid, Kevin Yondan, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Salum Abubakar, John Bocco, Mwinyi Kazimoto/Shaaban Nditi na Simon Msuva/Amri Kiemba.
Burundi; Arthur Arakaza, Gilbert Kaze, Haruna Manirakiza, Hassan Hakizimana, Emery Nimubona, Yussuf Ndikumana, Steve Nzigamasabo, Chris Nduwarugira, Suleiman NdikumanaChris Ndayishimiye na Amisi Tambwe.

Comments