MILOVAN AACHA WOSIA MZITO KUHUSU BOBAN


KOCHA mkuu wa Simba Mserbia Milovan Cirkovic ameutaka uongozi wa timu kuhakikisha inambakiza kundini kiungo wake aliyesimamishwa, Haruna Moshi ‘Boban’. 
Boban pamoja na beki wa timu hiyo Juma Nyoso ambao walisimamishwa hivi karibuni kutokana na utovu wa nidhamu. 
Kiongozi mmoja wa Simba aliliambia gazeti hili jana kwa Milovan alitoa wosia huo muda mfupi kabla ya kutimkia kwao Serbia  kwa mapumziko na kusema kwamba Boban ni mchezaji mzuri hivyo Simba kama itamtosa itakuwa imepoteza lulu. 
Alisema Milovan hakuna mchezaji kama Boban katika ukanda wa Afrika Mashariki na hilo alilibaini kupitia michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame iliyofanyika nchini mwezi Agosti na Yanga kutwaa ubingwa . 
“Kocha alituambia hata kama tutaamua kuachana naye lakini tusimuache Boban kwani ni mchezaji mzuri na kasoro alizonazo ni za kibinadamu tu…kikubwa ni uongozi kutochoka kwa kumjenga kisaikolojia tu,”alisema kiongozi huyo. 
Tayari uongozi wa Simba umeshawapa barua za kuwataka kujieleza wachezaji hao na ndipo watatoa uamuzi dhidi yao. 
Hata hivyo kuna taarifa za Nyoso kupelekwa kwa mkopo Coastal Union ya Tanga huku Boban akitarajiwa kurejeshwa kundini si tu kwa ajili ya uwezo alionao bali kukikingiwa kifua na baadhi ya watu wenye nguvu ndani ya klabu hiyo. 
Uongozi wa Simba ambao kwa sasa upo katika shinikizo la kutakiwa kujiuzulu na wanachama kutokana na mwenendo mbaya wa timu kwenye mzunguko wa kwanza uliomalizika kwa kushika nafasi ya tatu nyuma ya Azam Fc na Yanga inayoongoza,  utakutanana wakati wowote kujadili suala hilo.