KILIMANJARO MARATHON 2013 YAZINDULIWA RASMI


Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Bi. Kushilla Thomas akishirikiana na Mkurugenzi Msaidizi wa Michezo wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Bi. Juliana Yassoda kukata utepe kuzindua rasmi mbio za Kilimanjaro Marathon 2013 zinazotarajiwa kufanyika Moshi mwezi Machi mwaka 2013. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki. (Picha: Executive Solutions)

PRESS RELEASE

Mbio za 11 za Kilimanjaro Marathon zinazotarajiwa kufanyika tarehe 3 Machi 2013 huko Moshi zimezinduliwa.
Akiongea kwenye uzinduzi huo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Bi. Kushilla Thomas alisema bia ya Kilimanjaro Premium Lager inaendelea na udhamini wa mbio hizo zinazoendelea kuwa kubwa na bora kila mwaka huku zikiibua vipaji vipya na kuwapa wanariadha chipukizi fursa ya kukua na kuweza kushindana kimataifa.
“Kilimanjaro Premium Lager inalenga kuendeleza riadha kwa kukuza vipaji, kuwapa wanariadha wetu jukwaa la kushindania na wanariadha kutoka mataifa mbalimbali.” Alisema Kushilla.
Aliongeza kuwa bia ya Kilimanjaro Premium Lager ina lengo la kuhakikisha mashindano hayo yanakuwa na mvuto kwa wanariadha wenye vipaji ili kuongeza ubora wa riadha ya Tanzania ili Watanzania waweze kushiriki kikamilifu kwenye mashindano makubwa duniani.
Kwa upande wake, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema: “Kupata washiriki kutoka nchi mbalimbali inatusaidia kuonyesha dunia kuwa Kilimanjaro Marathon nini lakini kuwaendeleza na kuwapa moyo wanariadha Watanzania ni kipaumbele chetu kikubwa, kwa sababu hiyo tumeanzisha zawadi maalum ya shilingi milioni 3 kwa Watanzania watakaomaliza wakiwa wa kwanza katika mbio za 42km Kilimanjaro Premium Lager Marathon na hii ni mbali na zawadi watayopata kwa nafasi watakazoshinda.”

“Maandalizi ya Kilimanjaro Marathon 2013 yameishaanza ili kuhakikisha mbio hizo zinakuwa bora kama ilivyo utamaduni wetu kuhakikisha tunaboresha kila mwaka ili kuwapa raha ya aina yake washiriki pamoja na watazamaji.”
 “Kwa mara nyingine tena, Kilimanjaro Premium Lager itaendelea kuwathamini wanariadha kwa kuwatunuku zawadi nzuri ya fedha taslimu huku ikiwapa watazamaji burudani ya aina yake.”
Zawadi ya fedha taslimu kwa washindi wa kwanza hadi wa tatu wanaume kwa wanawake kwenye mbio ndefu za km 42.195 zijulikanazo kama Kilimanjaro Premium Lager Marathon itakuwa ni shilingi milioni 3 , washindi wa pili watajipatia shilingi milioni 1.5 kila mmoja huku washindi wa tatu wakijipatia shilingi 850,000 kila mmoja. Zawadi nhii itakuwa ni kivutio kwa wanariadha mashuhuri kushiriki katika mbio hizi zinazoingia mwaka wa 11 tangu kuanzishwa.