KIKOSI STARS CHATAJWA, KASEJA NA SAMATTA NDANI


Kim kushoto akiwa na kocha wa vijana, Jacob Michelsen
 Na Princess Asia, Mwanza
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark Kim Paulsen amemuorodhesha kipa Juma Kaseja katika kikosi cha wachezaji 22 watakaounda kikosi cha Bara, Kilimanjaro Stars kitakachomenyana na Kenya, Harambee Stars katika mchezo wa kirafiki ulio katika kalenda ya FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wiki ijayo.
Mbali na Kaseja wa Simba, Kim aliyepandishwa kutoka timu ya vijana mwaka huu akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Borge Poulsen amemuita pia kipa Deogratius Mushi wa Azam FC.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Mwanza leo, Paulsen aliwataja wachezaji wengine ni mabeki Kevin Yondan wa Yanga, Aggrey Morris, Erasto Nyoni wa Azam FC, Issa Rashid, Nassoro Masoud ‘Cholo’, Shomari Kapombe na Amir Maftah wa Simba, wakati viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wa Azam FC, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Mrisho Ngassa wa Simba, Athuman Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo wa Yanga na Shaaban Nditi wa Mtibwa Sugar.
Washambuliaji walioitwa na Paulsen ni John Bocco ‘Adebayor’ wa Azam FC, Simon Msuva wa Yanga, Christopher Edward wa Simba, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Hata hivyo, Poulsen hakuchukua wachezaji wa Zanzibar kwa sababu nao watakwenda kujiunga na timu ya Zanzibar, inayojiandaa na michuano ya Kombe la CECAFA Tusker Challenge mwishoni mwa mwezi huu mjini Kampala, Uganda. Alisema hicho ndio kikosi anachotarajia kukutumia katika Challenge. Kambi ya timu hiyo itakuwa mjini Mwanza, kwa kuwa ni jirani na Uganda.

Comments