HAWA NDIO WATAKAOWANIA UONGOZI DRFA, MAYAY , NTAHILAJA WAREJESHWA

Mwenyekiti wa kamati ya Uchaguzi ya DRFA, Juma Simba akitangaza majina ya wadau waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika chama hicho.


HATIMAYE wagombea  23 wamepitishwa kuwania uongozi katika Uchaguzi wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), unaotarajiwa kufanyika Desemba 12, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya DRFA, Juma Simba, a majina hayo yamepitishwa baada ya kufanyika usaili pamoja na kujadili pingamizi na rufaa zilizowasilishwa.

Alisema awali wagombea 36 walijitokeza na kuomba nafasi mbalimbali, kabla ya wengine kuenguliwa ama kujitoa katika kinyang’anyiro kwa sababu mbalimbali. 
Aliwataja waliopitishwa kuwania nafasi ya uenyekiti ni pamoja na  Ayoub Nyenzi, Evans Aveva, Brown Ernest na Almasi Kasongo, huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti itawaniwa na Meba Ramadhan, Salum Mwaking'inda, Gungurungwa Tambaza na Ally Mayai.
 Kwa upande wa nafasi ya Katibu watakaochuana ni pamoja na  Msanifu Kondo na Khamis Ambari, huku waliopitishwa kuwania  nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania ni Shafii Dauda, Muhsin Balhabouh na Shufaa Jumanne. 
“Wanaowania ujumbe wa kamati ya utendaji ni Shaban Kupasya, Siza Chenja, Sunday Mwanahewa, Hamis Kisiwa, Franck Mchaki na Baraka Mapande wakati watakaowania ujumbe kuwakilisha klabu ni Benny Kisaka, Juma Pinto, Frank Mchaki na Philemon Ntahilaja”, alisema 
Aidha, Simba aliwataja wajumbe ambao wamechujwa ni Salum Mkemi na Juma Jabir (Uenyekiti), Issac Mazwile (Makamu Mwenyekiti), Said Tully na Kassim Mustaffa (Katibu Mkuu), Isaack Mazwile (Mjumbe Mkutano Mkuu TFF) na Chano Karaha (Mjumbe Kamati ya Utendaji).