HASANOO ATINGA MAHAKAMA KUU


Hasanoo

Na Happiness Katabazi 
MWENYEKITI wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (Corefa), Hassan Othman maarufu kama Hasanoo (43) na wenzake watano ambao wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la uhujumu uchumi na kusafirisha pembe za ndovu zenye thamani ya sh bilioni 1.1 kwenda Hong Kong, China katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana aliwasilisha ombi la kuomba dhamana na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Hassanoo ambaye anatetewa na wakili wa kujigetemea Richard Rweyongeza, ndiye aliyewasilisha maombi hayo kwa njia ya maandishi kwa niaba ya mshtakiwa huyo anayesota gerezani tangu alipofikishwa katika mahakama ya Kisutu Ijumaa iliyopita akikabiliwa na kesi hiyo mpya ya kusafirisha pembe za ndovu.
Wakili Rweyongeza, alifikia hatua ya kuwasilisha ombi hilo jana kutokana na mahakama ya Kisutu kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo,  pia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, hakutoa kibali cha kuruhusu kesi hiyo isikilizwe katika Mahakama ya Kisutu.
Novemba 23 mwaka huu, siku ambayo kesi hii ilifunguliwa, Wakili Mwandamizi wa  Serikali, Shedrack Kimaro mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mbando, alidai kuwa mbali na Hassanoo, washtakiwa wengine ni Ally Kimwaga, Dastan Mwanga, Godfrey Mwanga, John Mlay na Khalid Fazaldin.
Kimaro alidai, shtaka la kwanza ni la kula njama na kujihusisha na biashara haramu ya kusafirisha nyara za serikali bila leseni ambalo walilitenda  kati ya Septemba Mosi na Novemba 20, mwaka huu, Dar es Salaam na Hong Kong kinyume na kifungu cha 384  cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Katika shitaka la pili, washtakiwa hao kwa nia ovu walipanga, wakatekeleza, wakasimamia na kuwezesha  kifedha kufanyika kwa biashara hiyo haramu ya kutorosha vipande 569 vya pembe za ndovu, vyenye uzito wa kilo 1330 na thamani ya sh 1,185,030,000 kwenda Hong Kong, kosa ambalo walilitenda kati ya Septemba Mosi na Novemba 20 mwaka huu, kusafirisha nyaraka hizo kutoka Dar es Salaam kwenda Hong Kong.
Aidha, alidai shtaka la tatu kuwa, siku hiyo ya tukio, washtakiwa walijihusisha na biashara hiyo ya nyara za serikali  kinyume na kifungu cha 80 na 34 ya uhifadhi wa Wanyama Pori namba 5.
Aliongeza kwa kudai kuwa, washtakiwa hao kwa nia ovu waliendesha biashara hiyo ya nyara za serikali bila ya kuwa na kibali halali kinachowaruhusu kufanya biashara hiyo.
Mbali ya kesi hiyo, Hasanoo aliyewahi kuwa Katibu wa Klabu ya Simba, pia anakabiliwa na kesi nyingine ya wizi wa tani 26.475 za madini aina ya Shaba
zenye thamani ya sh 333, 467,848.13 kutoka Zambia kinyume na kifungu cha 258, 265 na 269 (c) vya kanuni ya adhabu, mali ya Kampuni ya Liberty Express Tanzania Ltd ambayo ilifunguliwa mahakamani hapo mwaka jana na imefikia hatua ya kuanza kusikilizwa.