BRIDGIT NDIYE MISS TANZANIA 2012

MTOTO WA SINZA AWA MISS TANZANIA 2012

Bridgit katikati akiwa na washindi wake wa pili na wa tatu baada ya shindano usiku jana

Na Princess Asia
KIMWANA Bridgit Alfred mwenye umri wa miaka 18, amefanikiwa kutwaa taji la Miss Tanzania 2012 usiku wa kuamkia leo katika shindano lililofanyika kwenye ukumbi wa Blue Pearl Hotel, uliopo ndani ya jengo la Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, kimwana huyo kutoka Kinondoni, Dar es Salaam katika kitongoji cha Sinza, amezawadiwa Sh. Milioni 8 na gari ambalo aina yake na thamani yake vitajulikana baadaye.
Mshindi wa pili Euegene Fabian anapewa Sh. Milioni 6.2 na wa tatu Eddah Sylvester anapaewa Milioni 4.
Washijdi wengine, wa nne Milioni 3, wa tano Milioni 2.4 na wa sita hadi 15 kila mmoja atapata Milioni 1.2, wakati washiriki wengine kila mmoja atapata kifuta jasho cha Sh. 700,000.
Mapema mwaka huu, Kamati hiyo iliendesha shindano dogo na kumpata Lissa Jensen ambaye aliwakilisha nchi katika fainali za Dunia kutokana na mabadiliko ya kalenda yaliyofanywa na Kamati ya Miss World na mrembo atakayetwaa taji hilo katika fainali hizo zitakazofanyika hivi karibuni atapata muda mrefu wa kufanya maandalizi.
Shindano la Miss Tanzania lilianza rasmi mwaka 1994 na Aina Maeda alikuwa mshindi wa kwanza, akifuatiwa na Shose Senare 1995, Emily Adolf 1996, Saida Kessy 1997, Basila Mwanukuzi 1998, Hoyce Temu 1999, Jacqueline Ntuyabaliwe 2000, Happiness Magese 2001, Angela Damas 2002, Sylvia Bahame 2003, Faraja Kotta 2004, Nancy Sumary 2005, Wema Sepetu 2006, Richa Adhia 2007, Nasreem Kareem 2008, Miriam Gerald 2009, Geneveive Mpangala 2010 na Salha Israel 2011.
Awali ya hapo, mwaka 1967 lilifanyika shindano la kwanza kabisa la Miss Tanzania na Theresa Shayo akashinda katika shindano lililofanyika kwenye bwawa la kuogelea la hoteli ya Kilimanjaro, lakini serikali ya Tanzania wakati huo, chini ya rais wa kwanza, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikapiga marufuku mashindano kwa sababu hayaendani na mila na desturi za Mtanzania.
Lakini Lino International Agency, ikajenga hoja ambazo ziliishawishi serikali ya Tanzania, chini ya rais wake wa pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi kuruhusu mashindano hayo yafanyike tena, ingawa mwaka 2001 yaliponea chupuchupu kufutwa tena, enzi za rais wa awamu wa tatu, Benjamin William Mkapa.
Ilitokana na vazi la kuogelea ‘kichupi’, ambalo lilipingwa kwa sababu linamdhalilisha mwanamke wa Tanzania, lakini Lino ikaboresha kipengele cha vazi hilo, kutoka la kuogelea hadi la ufukweni, ambalo kidogo linamsitiri binti na serikali ikaruhusu mashindano yaendelee.
Hata hivyo, mabinti wanapokwenda kwenye shindano la dunia, wanavaa vazi la kuogelea kupanda jukwaani, katika shindano ambalo linaonyeshwa moja kwa moja nchi zaidi ya 100 duniani na picha zao kuchapishwa kwenye majarida, magazeti na mitandao mbalimbali duniani.
Bridgit sasa atashiriki shindano la Miss World mwakani, baada ya Lisa kushiriki mwaka huu na kuanzia sasa atakuwa akiandaliwa kwa ajili ya fainali hizo. 

Comments