AZAM YAZINDUKA, YAIPIGA 4-1 COASTAL


Mwaikimba na Samir Hajji Nuhu wakipongezana. Habari na picha kwa hisani ya bongostaz.blogspot.com
 KOCHA Muingereza Stewart Hall amerejea na ‘bonge la zali’, baada ya leo kuiongoza timu hiyo kuichapa Coastal Union ya Tanga mabao 4-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Stewart alitua jana usiku Dar es Salaam akitokea Kenya alipokuwa anaifundisha Sofapaka ya Ligi Kuu ya huko, baada ya kufukuzwa Azam Agosti mwaka huu na leo ameanza kazi, akirithi mikoba ya Mserbia, Boris Bunjak aliyefukuzwa Jumatatu.
Kwa ushindi huo, Azam imefikisha pointi 21, baada ya kucheza mechi 10 na sasa inarejea nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Simba na Yanga, zenye pointi 23 zote baada ya kucheza mechi 11, kila timu.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Simon Mbelwa, aliyesaidiwa na Abdallah Rashid wote wa Pwani na Michael Mkongwa wa Njombe, hadi mapumziko Azam tayari walikuwa wanaongoza kwa mabao 3-0.
Gaudence Mwaikimba aliifungia Azam bao la kwanza kwa kichwa dakika ya 23 kabla ya Kipre Tcheche kufunga la pili dakika ya 36, baada ya kuipasua ngome ya Coastal na Khamis Mcha ‘Vialli’ akafunga la tatu dakika ya 44.
Coatsal walianza vizuri mechi hiyo na kusukuma mashambulizi langoni mwa Azam, lakini baada ya dakika 20, wakapoteza mwelekeo na kuanza kuwaruhusu wapinzani wao kuvuna mabao. 
Kipindi cha pil, Azam walirudi na moto wao, lakini kidogo Coastal walibadlika nao na kufanya mchezo uwe mgumu kidogo.
Hata hivyo, walikuwa ni Azam tena waliotikisa nyavu za Coastal, baada ya kiungo Othman Tamim kujifunga dakika ya 73 katika harakati za kuokoa.
Baada ya bao hilo, Coastal walizinduka na kuanza kushambulia kupitia pembeni, jambo ambalo liliwasaidia kupata bao la kufutia machozi lililofungwa ma kiungo Jerry Santo.
Kwa ujumla katika mchezo wa leo, Coastal walizidiwa katika safu ya kiungo ambako leo Stewart alipanga viungo wengi waliotekeleza majukumu yao vyema.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Coastal, Hemed Morocco alisema kwamba walizidiwa uwezo na wapinzani wao na kwa ujumla vijana wake walicheza chini ya kiwango leo, hata hivyo anakwenda kufanyia kazi makosa ili timu irejeshe makali yake.
Stewart alisema anafurahi kukaribishwa na ushindi huo mnono na kwamba hizo ni dalili njema. Aliwapongeza vijana wake kwa kucheza kwa kufuata maelekezo yake na akasema kwamba sasa anaelekeza nguvu zake katika mchezo ujao dhidi ya Yanga Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.  
Azam FC; Mwadini Ally, Samir Hajji, Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris, Said Mourad, Kipre Balou/Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aziz, Salum Abubakar/Himid Mao, Gaudence Mwaikimba/Abdi Kassim, Kipre Tcheche na Khamis Mcha ‘Vialli’.
Coastal Union; Jackson Chove, Said Swedi, Juma Jabu, Mbwana Hamisi, Jamal Machelanga/Salim Gilla, Jerry Santo, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Razack Khalfan/Hamisi Shango, Daniel Lyanga, Atupele Green/Lameck Dayton na Othman Tamim.

Comments