YANGA YASISITIZA KUTOVAA JEZI ZA VODACOM, YAPIGWA FAINI


Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako

WAKATI klabu ya Yanga ikisisitiza kuendelea kutovaa jezi za wadhamini Wakuu wa Ligi kuu Bara, kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, Shirikisho la soka Tanzania (TFF) litaipiga faini ya shilingi Mil.1.5 timu hiyo kutokana na kutovaa jezi zenye nembo hiyo.

Yanga na African Lyon zilivaa jezi isiyo na nembo ya Vodacom zilipomenyana juzi katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
  Ofisa TFF Boniface Wambura alisema kwamba Yanga na Lyon itaadhibiwa kwa mujibu wa kanuni ya 8 kifungu  kidogo cha 38 kintoa adhabu ya faini hiyo kutokana na kosa hilo.

Alisema adhabu hiyo ya pia itavikumba vilabu vingine ambavyo vitajaribu kufanya mambo ambayo yapo kinyume na mkataba wa wadhamini wa ligi hiyo.

Awali, Katibu Mkuu wa Yanga Lawrance Mwalusako alisema kwamba wataendelea kuvaa jezi nzisizo na nembo ya Vodacom mpaka pale wadhamini wao watakapotatua tatizo lao kwani hawako tayari kuvaa kitu chenye doa jekundu.

Alisema sakata hilo lilianza tangu msimu uliopita wa ligi hiyo ambapo baada ya mazungumzo na wahusika walikubalina kuondoa doa hilo kwenye logo watakayotumia lakini cha kushangaza wameshindwa kufanya hivyo.

“Hatukufanya makusudi kuvaa jezi tulizopewa na wadhamini bali hatuwezi kuvaa jezi zenye doa jekundu…sisi tunatumia rangi ya njano, kijani au nyeusi lakini si nyingine hivyo wahusika inabidi walitatue jambo hilo,”alisema.

Mwalusako aliongeza kuwa tayari wameiandikia barua TFF kuikumbusha juu ya suala hilo na wanaimani litashughul;ikiwa ipasavyo ili kuondoa hisia tofauti zilizojengeka vichwani mwa watu.