YANGA YAICHAPA TOTO 3-1

Na Prince Akbar, Mwanza
YANGA SC leo imezinduka baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Toto African, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Matokeo haya, yanaifanya Yanga itimize pointi 11, katika mechi saba ilizocheza hadi sasa, ikiwa imefungwa mbili, sare mbili na kushinda tatu, inazidiwa pointi tano na wapinzani wake wa jadi, Simba SC wanaoongoza ligi hiyo kwa pointi zao 16, wakifuatiwa na Azam wenye pointi 13.
Hadi mapumziko, Yanga walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-0, yaliyopachikwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu na beki wa kimataifa wa Rwanda, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbuyu Twite.
Kavumbangu alifunga bao la kwanza dakika ya pili, baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Erick Ngwengwe kufuatia kona iliyochongwa na Haruna Niyonzima, hilo likiwa bao lake la tano ndani ya mechi 11 tangu ajiunge na Yanga msimu huu akitokea Atletico ya kwao, Burundi.
Baada ya bao hilo, Yanga waliendelea kulisakama lango la Toto na dakika ya 21, Mbuyu Twite akaunganisha kona ya chini chini iliyochongwa na Niyonzima.
Toto ilipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 42, baada ya kupata penalti, kufuatia beki mmoja wa Yanga kuunawa mpira kwenye eneo la hatari, baada ya Wana Kishamapanda kufanya shambulizi kali la kushitukiza, lakini kiungo Emanuel Swita akapiga nje.
Swita alipiga penalti nzuri tu ya chini pembeni kabisa, lakini vipimo vyake vikazidi kidogo, mpira ukatoka nje, ingawa Berko aliifuata vizuri pembeni kabisa kulia kwake na angeweza kuokoa.
Kipindi cha pili Toto waliingia kwa kasi zaidi na kuanza kulishambulia lango la Yanga mfululizo, wakitawala zaidi sehemu ya kiungo.
Katika dakika ya 54 mshambuliaji Mussa Said aliifungia Toto bao safi, baada ya kipa Yaw Berko kutoka langoni.
Baada ya bao hilo, Toto walizidi kutawala mchezo na kukosa mabao mawili ya wazi- hapo ndipo kocha Mholanzi, Ernie Brandts akawatoa viungo Frank Domayo na Athumani Idii ‘Chuji’ na kuwaingiza Shamte Ally na David Luhende.
Walipoingia Shamte na Luhende wote walienda kushambulia pembeni na Haruna Niyonzima na Nurdin Bakari wakarudi katikati.
Mabadiliko hayo yaliisaidia Yanga kupata bao la tatu dakika ya 68, lililofungwa kitaalamu na mshambuliaji Jerry Tegete ambaye alimpiga chenga kipa Ngwengwe baada ya kupokea pasi ya Oscar Joshua.  
Baada ya bao hilo, Kocha wa Toto, Johh Tegete naye alifanya mabadiliko akiwatoa Mussa Said na Evarist Maganga na kuwaingiza Heri Mohamed na Heri Kyaruzi. Hata hivyo, pamoja na mabadiliko hayo, Yanga waliendelea kutawala mchezo hadi filimbi ya mwisho.
Kwa ushindi huu, Yanga imelipa kisasi cha mara ya mwisho timu hizo, zilipokutana kwenye Uwanja huo, Jumapili ya Aprili 15, mwaka huu, Toto walipoibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Yaw Berko, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’/Shamte Ally, Frank Domayo/David Luhende, Haruna Niyonzima, Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Nurdin Bakari.
Toto; Erick Ngwengwe, Kulwa Greyson, Eric Mulilo, Evarist Maganga/Heri Kyaruzi, Peter Mabula, Hamisi Msafiri, Emanuel Swita, Haroun Athumani, Mohamed Hussein, Suleiman Kibuta na Mussa Said/Heri Mohamed.  

Comments