YANGA YAENDELEA KUTESWA KAGERA,YAPIGWA 1-0


Na Ashura Jumapili, Bukoba

MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga ya jijini Dar es Salaam ilikubali kipigo cha pili katika mfululizo wa Ligi Kuu Bara, baada ya kulala kwa bao 1-0 mbele ya wakata miwa wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba jana.
Katika pambano hilo lililochezeshwa na mwamuzi Omari Juma kutoka Mwanza, timu zote zilianza mchezo kwa tahadhari na kushambulia kwa zamu, ambako dakika ya 20, mshambuliaji mahiri wa Yanga, Said Bahanuzi aliumia baada ya kuanguka na nafasi yake kuchukuliwa na Jerry Tegete, kabla ya dakika ya 44 Benjamin Efe wa Kagera Sugar naye kupata maumivu na kutoka.
Hadi filimbi ya mwamuzi Juma kuashiria mapumziko, hakuna nyavu iliyokuwa imetingishika.
Kipindi cha pili, kilianza kwa kasi na dakika ya 52, Frank Domayo wa Yanga, alilimwa kadi ya njano na dakika ya 64, George Kavilla wa Kagera naye alizawadiwa kadi hiyo.
Alikuwa ni mtokea benchi, Themi Felix dakika ya 67, alipowainua mashabiki wa Kagera Sugar kwa kupachika bao pekee la ushindi kwa shuti baada ya mabeki wa Yanga kujichanganya na kipa Yaw Berko kutoka langoni.
Yanga ambao walishuka Kaitaba wakiwa na Kocha wao mpya, Ernts Brants raia wa Uholanzi, wakiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 na watani zao Simba Jumatano iliyopita kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam, ilipigana kutaka kusawazisha, lakini hadi dakika 90 zinakamilika, Kagera Sugar iliibuka na ushindi huo wa bao moja.
Kipigo hicho ni cha pili tangu ligi hiyo ianze Septemba 15, ambako cha kwanza ilikubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa wakata miwa wa Manungu, Turiani Morogoro, Mtibwa Sugar.
Kwa matokeo hayo, Yanga imebaki na pointi zake nane, tofauti pointi nane na vinara wa ligi hiyo Simba, wenye pointi 16 huku Kagera Sugar ikizidi kupaa na kufikisha pointi 10 zote zikiwa zimeshuka dimbani mara sita.
Yanga: Yaw Berko, Jumja Abdul, Stephano Mwasika, Nadir Haroub ‘Canavaro’, Mbuyu Twite, Athumani Idd ‘Chuji’, Nizar Khalfan, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Said Bahanuzi/Jerry Tegete na Haruna Niyonzima.
Kagera Sugar: Andrew Mtala, Jumanne Nade, Salum Kanoni, Benjamin Efe, Amandus Nesta, Maregesi Mwangwa, Daud Jumanne, Enyina Darlington/Themi Felix, Shija Mkina, Wilfred Ammeh.