YANGA WALIA MAPATO KIDUCHU MECHI YAO NA SIMBA


KLABU ya Yanga imeeleza kusikitishwa kwa kutangzwa kwa mapato kiduchu katika mechi yao dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba na kulitaka Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kulifanyia uchunguzi wa kina suala hilo.

Hatua hiyo inafuatia TFF kutangaza mapato ya sh. milioni 390, 568,000 ambayo yalitokana na watazamaji 50,455 waolikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa usiku kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
 Katibu Mkuu wa Yanga Lawrance Mwalusako alisema kwamba hali hiyo inatia shaka kwani hata takwimu za idadi ya watazamaji zilizotolewa na TFF ni tofauti na ile ya kituo cha  Televisheni cha  Supersport ambacho kilionyesha kuwa lilihudhuriwa na mashabiki 59000. 
Alisema kwa hesabu za haraka haraka hata mashabiki waliohudhuria mechi hiyo wangelipa 15,000 kila mmoja zingepatikana zaidi ya shilingi milioni 600 hivyo hata vilabu husika vilistahili kupata zaidi ya milioni 93,345,549.15  walizogawiwa kila klabu kama sehemu ya mapato hayo.
 Mwalusako aliongeza kwamba wanashindwa kuelewa hali hiyo inatokana na nini na kuiomba TFF kufanya uchunguzi wa haraka ili kujua tatizo linatoka wapi, lakini kinyume na hapo hali itazidi kuwa mbaya. 
Katibu huyo aliongeza kuwa wanatarajiwa kuwasiliana na viongozi wenzao wa Simba ili kujadili hali hiyo kabla ya kutoa tamko la pamoja.