YANGA KUZOA POINTI TATU KWA TOTO LAO LEO?


MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga ya jijini Dar es Salaam leo inatarajiwa kushuka kwenye dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza kuwavaa wenyeji Toto African katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom.
Yanga itashuka uwanjani ikiwa bado na maumivu ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar ya Kagera mjini Bukoba Jumatatu.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako, alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba, baada ya kipigo cha Kagera, wamefanyia kazi upungufu uliojitokeza na anaamini watashinda leo.
Alisema zaidi ya kuwaweka sawa wachezaji kwa ajili ya mchezo huo, pia wamewajenga kisaikolojia ili waweze kusahau ya Kagera na kuelekeza nguvu katika michezo mingine ya ligi hiyo.
“Mchezo ni mchezo lazima kuwepo na upinzani, hivyo nasema utakuwa ni mgumu…kikubwa ni kuwa tumejipanga katika kila idara kuhakikisha tunaondoka na pointi tatu,” alisema.
Katika mchezo wa leo, Yanga itawakosa nyota wake muhimu wakiwemo beki Kelvin Yondani pamoja na Said Bahanuzi ambao ni majeruhi.
Yanga hivi sasa inakamata nafasi ya nane katika msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 8 baada ya kushuka dimbani mara sita.