WASANII WANAOKIUKA MAADILI NCHINI KUANZA KUSHUGHULIKIWA


Na Mwandishi wetu
 
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewaagiza viongozi wa Mashirikisho ya sanaa hapa nchini kufuatilia kwa karibu matukio ya ukiukwaji wa maadili yanayoendelea katika Sanaa hivi sasa na kuchukua hatua kwa wnaobainika kufanya hivyo.
 
Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego,  mbali na BASATA kuwakemea vikali wasanii wanaotumia majukwaa kwa kuidhalilisha Sanaa wao wenyewe na watazamaji pia limeyataka mshirikisho kushirikiana na vyama vyao kuwaita wale wote watakaohusika na uvunjwaji wa maadili ili kuwakanya katika hatua ya kwanza na kama wasipoacha tabia hizo Baraza litawafungia kujishughulisha na kazi ya Sanaa  hapa nchini.
 
“Shirikisho la Muziki tumeliagiza kuangalia tungo za wanamuziki zenye maneno yenye lugha isiyofaa, Shirikisho la Sanaa za Ufundi limeagizwa kuwachukulia hatua wasanii wachoraji na wachongaji wanaotengeneza Sanaa zinazokiuka maadili. Aidha Shirikisho la Sanaa za Maonyesho waliagizwa kufuatilia wasanii wote wanaocheza bila staha majukwaani. Na mwisho Shirikisho la Filamu tumeliagiza kuwaita, kuwaonya na kuwachukulia hatua wasanii wote katika fani ya Filamu wanaovaa nusu utupu bila kuzingatia husika katika kazi za Sanaa,” amesema Ghonche.
 
Aidha Baraza limewaagiza wamiliki wa kumbi zote za burudani kuzingatia maadili pale ambapo Sanaa zitakuwepo jukwaani na kwamba baraza halitasita kuufungia ukumbi wowote utakaokiuka agizo hilo.
 
“Pia tunaviomba vyombo vya usalama kuhakiki muda wa vibali vya maonyesho na bila kuchelewa kuwachukulia hatua stahiki wasiozingatia muda wa maonyesho. Na tunawakumbusha wamiliki wa vyombo vya Habari na Wahariri kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wasimamizi wa sanaa kwa kutokurusha wala kutangaza maonyesho ambayo kwa njia yoyote yanachangia mmomonyoko wa maadili ya Taifa letu,” alisema Ghinche.
 
 Kwa suala hili, Baraza linaziomba mamlaka zinazohusika na usimamizi wa uendeshaji wa vyombo vya habari nchini kuingilia kati na kuvichukulia hatua vyombo vya habari ambavyo kila siku vimekuwa mstari wa mbele kueneza wimbi la mmomonyoko wa maadili hapa nchini na kushusha hadhi ya Tasnia/Sekta ya Sanaa nchini.
 
 
Sanaa ni kazi na Sanaa ni kioo cha Jamii.

Comments