WABABE WA TWIGA STARS WACHEZEA KICHAPO AWC


Ethiopia ambayo iliinyima Tanzania (Twiga Stars) nafasi ya kucheza fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zinazochezwa Equatorial Guinea imeanza vibaya fainali hizo baada ya kufungwa mabao 5-0 na Ivory Coast.
Mechi hiyo ya kundi B ilichezwa juzi usiku (Oktoba 29 mwaka huu) Uwanja wa Nkoantoma ulioko mjini Bata, ambapo mpaka mapumziko Ethiopia ilikuwa imeshalala kwa mabao 2-0. Kwa ushindi huo Ivory Coast inaongoza kundi hilo kwa tofauti ya mabao dhidi ya Nigeria.
Nigeria ambao ni mabingwa watetezi waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Cameroon katika mechi iliyotangulia kwenye uwanja huo. Katika fainali saba zilizopita za AWC, Nigeria imeibuka mabingwa mara tano.
Ethiopia ambayo iliitoa Twiga Stars katika raundi ya mwisho ya mechi za mchujo za AWC kwa kushinda Addis Ababa na Dar es Salaam itacheza mechi yake ya pili Novemba Mosi dhidi ya Nigeria ambayo kama ikipoteza itakuwa imetolewa kwenye fainali hizo.
Katika mechi za ufunguzi za kundi A wenyeji Equatorial Guinea (Nzalang Nacional) waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Afrika Kusini (Banyana Banyana) kwenye Uwanja wa Malabo. Bao la washindi lilifungwa dakika ya 33 kwa kichwa na Gloria Chinasa.
Nayo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) licha ya kuwasili hapa siku ya mechi iliifunga Senegal bao 1-0 katika mechi nyingine ya kundi A. Bao la DRC lilifungwa dakika ya 74 kwa njia ya penalti na Lucie Nona.
Boniface Wambura
CAF Media Team, Malabo, Equatorial Guinea