TASWA YALAANI WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO KUTISHIWA MAISHA NA MASHABIKI WA YANGA


Amir Mhando, Katibu Mkuu wa Taswa

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
CHAMA cha Waandishi wa Habari za  Michezo Tanzania (TASWA), kimesikitishwa na taarifa za baadhi ya  waandishi wa habari za michezo kupewa vitisho wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ya kazi.
TASWA imepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya waandishi wa habari za michezo  wakidai baadhi ya wanachama wa Yanga a.k.a  ‘Makomandoo’ wamewapa vitisho kabla na baada ya mchezo kati ya Kagera Sugar na Yanga uliofanyika Jumatatu wiki hii Uwanja wa Kaitaba Bukoba.
Sekreterieti ya TASWA ilifanya mawasiliano ya haraka na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Onesmo Kapinga ambaye alikuwa mkoani Kagera na amethibitisha pasi na chembe ya shaka kwamba vitisho hivyo vimewanyima fursa ya kutekeleza majukumy yao ya kazi.
Tukio hili limetuhuzunisha sana kwa sababu licha ya kuwajengea hofu baadhi ya waandishi wa habari kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi kikamilifu, lakini linaweza kujenga chuki zisizo na msingi kati ya klabu hiyo na TASWA.
Wanachama na mashabiki wa klabu kubwa hapa nchini Simba na Yanga wakubali changamoto za viwanjani na wasitake kutafuta mahali pa kupeleka lawama zao pale wanapoona matokeo mabaya kwa klabu zao.
Si nia ya TASWA kutetea udhaifu kama upo kwa baadhi ya waandishi wa habari, lakini tunaona kwa malalamiko yanayotolewa na baadhi ya makomandoo hao kwa wanahabari si mazuri na hoja zao hazina mashiko ni kutapatapa.
Tunauomba uongozi wa Yanga uwakemee mashabiki wake waachane na mambo yasiyo na msingi ambayo hayana manufaa kwa klabu hiyo na ulimwengu wa soka hapa nchini. TASWA inataka wanahabari wawe huru kutekeleza majukumu yao na hilo tuna hakika litafanyika.
Kamati ya Utendaji ya TASWA inatarajiwa kukutana mwishoni mwa wiki ijayo kujadili suala hili la vitisho kwa wanahabari na pia itajadili masuala mbalimbali ikiwemo kutaja mkoa utakakofanyika Mkutano Mkuu wa mwaka wa chama.

Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
11/10/2012

Comments