SITA WAWEKEWA PINGAMIZI UCHAGUZI TWFA


Wagombea sita wa nafasi mbalimbali za uongozi katika Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) wamewekewa pingamizi na wadau wa mchezo huo. 
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TWFA, Ombeni Zavala, wagombea hao ni Joan Minja anayewania nafasi ya Mwenyekiti ambaye amewekwa pingamizi na wadau sita. Pia Isabellah Kapera ambaye anagombea uenyekiti amewekewa pingamizi moja. 
Wagombea watatu wa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) nao wamewekewa pingamizi. Wagombea hao ni Julliet Mndeme (pingamizi sita), Zena Chande (pingamizi nne) na Jasmin Soud mwenye pingamizi tatu. 
Naye Rahim Maguza anayewania ujumbe wa Kamati ya Utendaji amewekewa pingamizi moja. 
Licha ya pingamizi hizo, wagombea wote wanatakiwa kuhudhuria usaili wakiwa na vyeti vyao halisi vya kitaaluma utakaofanyika Oktoba 12, 13 na 14 mwaka huu kwenye ofisi za TFF zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 3 asubuhi.

Comments