SIMBA YAWAONYA WANAOMCHAFUA BOBAN


msemaji wa Simba,Ezekiel Kamwaga

KLABU ya soka ya Simba ipo mbioni kuvichukulia hatua za kisheria baadhi ya vyombo vya habari ikiwemo  mitandao ya kijamii ambayo inaendesha zoezi la  kumchafua kiungo wao, Haruna Moshi ‘Boban’ baada ya kumkwatua nyota wa Yanga, Kelvin Yondan katika mchezo baina ya timu hiyo jumatano iliyopita. 
Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga amesema kwamba anashangazwa na mchakato huo kwani  kitendo alichokifanya Boban ni sehemu ya mchezo na ndiyo maana mwamuzi alitoa adhabu iliyostahili.
"Hata  wachezaji wenyewe  walishalizungumza hilo na na kusameheana lakini baadhi ya mitandao imekuwa ikimuandika Boban kama amefanya tendo la unyama. 
Kamwaga alisema wanawasiliana na mwanasheria wao ili kulifanyia kazi suala hilo ambalo kama likifumbiwa macho linaweza kuleta athari kubwa kwa jamii.
Katika mchezo huo wa ligi kuu bara uliopigwa uwanja wa Taifa jijini dar es Salaam timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, huku Yondan akilazimika kuwa nje ya uwanja kwa wiki mbili kutokana na kuumizwa na Boban.