SIMBA YAENDELEA KUPIGWA DANADANA JUU YA FEDHA ZA TWITE


Twite
SAKATA la Simba kurejeshewa dola 32,000 za usajili wa beki wa kimataifa wa Yanga, Mbuyu Twite limechukua sura mpya baada ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kulirudisha tena kwa kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF. 
Hatua hiyo inafuatia kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa kuipa Yanga siku 21 kuirejeshea Simba fedha hizo, lakini mpaka kipindi hicho kinamalizika wiki iliyopita Yanga ilishindwa kutimiza maelekezo hayo. 
 Ofisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema kwamba baada ya kuona kimya kuhusiana na deni lao waliandika barua TFF ili kuomba msaada wa jambo hilo. 
Alisema TFF iliwataka kusubiri mpaka kamati ya kina Mgongolwa itakapoketi kwani ilibidi suala hilo walirejeshe tena katika kamati hiyo kutokana na awali kutotoa mwongozo nini kifanyike iwapo Yanga ingeshindwa kulipa deni katika siku ilizopewa. 
Kamwaga aliongeza kwamba wanasikitishwa na kitendo wanachokifanya Yanga kwani suala hilo halikupaswa kufikia hatua iliyopo sasa. 
Naye Katibu Mkuu wa Yanga Lawrance Mwalusako alipozungumza na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na suala hilo, alidai hawezi nkulizungumzia kwani lipo ndani ya uongozi wa klabu hiyo. 
Awali, Simba ilimsajili Twite kutoka klabu ya APR ya Rwanda ambayo alikuwa akiichezea kwa mkopo kutoa FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kwa dau la dola 32,000 kabla ya Yanga kumpandishia dau la dola 50,000 na hivyo kumwaga wino. 
Hata hivyo, Simba ilikuja juu kwa madai Yanga ilivuruga usajili huo, huku Yanga nayo ikitumia maarifa zaidi ya kufanya mazungumzo na uongozi wa Lupopo ambayo ndiyo yenye mamlaka na Twite na si APR kama ilivyofanya Simba. 
Kama hiyo haitoshi, baadhi ya viongozi wa FC Lupopo walikuja jijini Dar es Salaam ili kuwarejeshea Simba fedha zao lakini viongozi wa Simba waligoma na kudai hawakutoa fedha hizo kwa uongozi wa Lupopo hivyo wanataka Twite mwenyewe arudishe fedha hizo.