SIMBA SC, COASTAL UNION HAPATOSHI MKWAWANI LEO


MABINGWA watetezi na vinara Ligi Kuu ya Bara, Simba, leo wanashuka kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa kuwakabili Coastal Union katika mechi inayotarajiwa kuwa yenye ushindani mkubwa kwani wakali hao wa Msimbazi, watakuwa wakipigania ushindi ili kuendeleza rekodi ya kutofungwa.
Tangu kuanza kwa ligi hiyo Septemba 15, Simba imecheza mechi sita na kushinda tano na sare moja, hivyo kuongoza kwa pointi 16 huku Coastal Union ikiwa nafasi ya saba baada ya kujikusanyia pointi tisa katika mechi sita.
Kikosi cha Simba chini ya Mserbia Milovan Cirkovik, tayari kimewasili mjini humo tangu juzi kwa mechi hiyo ambayo itachezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa wa Pwani akisaidiwa na Godfrey Kihwili na Abdallah Uhako wote kutoka jijini Arusha.
Akizungumza mechi hiyo kutoka jijini Tanga, Meneja wa Simba, Nico Nyagawa, alisema kikosi kipo fiti kupigania pointi tatu kuendeleza wimbi la ushindi.
Nyagawa, nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, alisema licha ya ubora wa kikosi chao, wanataraji kupata upinzani mkali kutoka kwa Coastal Union kwani ni kati ya timu zenye kiwango kizuri kwenye ligi hiyo na ndiyo maana wamevuna pointi tisa kwenye mechi sita.
“Tupo vizuri katika kila idara…mechi itakuwa ngumu kwani Coastal nayo ni moja ya timu nzuri, lakini vijana wamekamia kushinda,” alisema Nyagawa.
Alisema Simba itawakosa nyota wake watano akiwemo Emmanuel Okwi aliyekwenda kuitumikia timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ inayojiandaa na mechi ya kuwania tiketi ya fainali za Mataifa ya Afrika, Mrisho Ngasa, Koman Keita, Kigi Makassy na Haruna Shamte ambao ni wagonjwa.
Naye Ahmed Khatib anaripoti kutoka Tanga kuwa, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego, amewataka wachezaji wa Coastal Union iliyopiga kambi kwenye Hoteli ya In by the Sea iliyopo eneo la Raskazone, kucheza kwa juhudi kubwa ili kushinda na kuwapa raha wapenzi na mashabiki wao na wakazi wa jiji hilo kwa ujumla.
“Nasema kutokana na maendeleo yenu mazuri katika mechi zilizopita, nimewaona ni wazuri na mna uwezo wa kushinda mchezo wa leo dhidi ya Simba bila kuangalia ukubwa wa timu husika,” alisema Dendego kabla ya kukabidhi kiasi cha sh 300,000 kwa wachezaji wa timu hiyo.
Akipokea fedha hizo, Nahodha wa Coastal Union, Said Sued, alimshukuru kiongozi huyo na kuahidi kucheza kwa juhudi kubwa ili kushinda mechi hiyo na kuzidi kujiweka kwenye nafasi nzuri katika vita ya kupigania ubingwa wa ligi hiyo inayofanyika chini ya udhamini wa Kampuni ya Vodacom-Tanzania.
Mechi nyingine leo itakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kwa Polisi Moro kuwakaribisha Azam FC. Inatarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa kwani wakati maafande wakitaka kushinda kuondoka mkiani mwa ligi hiyo, wapinzani wao watakuwa wakitaka kushinda kufikisha pointi 13. 
Kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, wenyeji Tanzania Prisons iliyo nafasi ya tano kwa pointi tisa watawakaribisha maafande wenzao wa JKT Orjoro, pia yenye pointi tisa.
Nayo Ruvu Shooting iliyo nafasi ya 11 kwa pointi sita, itakwaana na African Lyon kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi huku mabingwa mara mbili wa Ligi Kuu (1999 na 2000), Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.

Comments