SERIKALI YABARIKI SANAA KAMA AJIRA RASMI


Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ghonche Materego akizungumza jambo wakati akifunga jukwaa la sanaa, Kushoto kwakwe ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Kazi na Ajira ,  Haji Janabi.

Na Mwandishi Wetu
Serikali imesema inatambua kwamba Sanaa ni ajira rasmi licha ya kuwa sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuratibu, uongozi na kupewa kipaumbele katika mipango ya kimaendeleo na Serikali.
Akiwasilisha mada ya Umuhimu wa Tasnia ya Sanaa katika kukuza Ajira nchini, katika Jukwaa la Sanaa, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Kazi na Ajira,  bwana Haji Janabi amesema sanaa ina mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza upatikanaji wa nafasi za ajira na kipato.
“Kwa Tanzania iwapo tutatumia vyema uwepo wa ubunifu muafaka katika sekta ya sanaa zetu bila shaka tasnia  hii inaweza kuchangia sana upatikanaji wa nafasi za ajira na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuondoa tatizo la ajira hapa nchini,” alisema Janabi.
Janabi amesema kwamba pamoja na hivyo kuna changamoyo kubwa ya kiuratibu na kimuundo ikiwa ni pamoja na Serikali kutotoa kipaumbe katika masuala yanayohusu sanaa na wasanii pamoja na mgongano wa kimamlaka kati ya vyombo vinavyohusika na uratibu wa masuala ya sanaa.
Aidha amesema pamoja na nafasi nzuri ya kukuza ajira, ujio wa teknolojia umeanza kubana soko la ajira ya sanaa ambapo kwa sasa teknolojia inapunguza uhitaji wa watu katika ufanyikaji wa sanaa kwa akitolea mfano katika muziki ambapo vitu vingi vinafanywa na mtu mmoja hivyo kupunguza nafasi za watu wengine.
Pia amesema ili sekata hii iweze kuwa ajira nzuri zaidi ni muhimu kukaandaliwa viwango na vigezo kama ilivyo kwa fani zingine  ili kuwe na maradaja ya wafanyaji kazi kulingana na viwango vya umahiri na taaluma. 

Comments